Ngajilo aingia tena uwanja wa Iringa Mjini kugombea ubunge

 Fadhili Fabian Ngajilo, mwanasiasa mwenye rekodi ya utumishi wa muda mrefu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo amechukua rasmi fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa mara ya tatu.

Amesisitiza kuwa safari yake ya kisiasa bado haijafikia mwisho na kuwa sasa ni wakati wa kulitumikia jimbo hilo kwa nguvu mpya na uelewa mpana wa changamoto zake.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu katika ofisi ya CCM wilaya ya Iringa Mjini, Ngajilo aliushukuru uongozi wa chama kwa kumpa nafasi ya kuendelea kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia na kueleza kuwa anaamini hakuna chama kingine kinachoweza kuleta maendeleo ya kweli kwa Watanzania isipokuwa CCM.

Aidha amadai kuwa ameamua kuchukua fomu kwa mara ya tatu, si kwa sababu ya tamaa, bali kwa sababu ya wito wa dhati wa kulitumikia jimbo langu. CCM ni chama makini chenye dira na msimamo wa maendeleo; nami ni sehemu ya mfumo huo kwa miaka zaidi ya 20.

Ngajilo ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Iringa, tayari ameandika barua kwa chama kuachia nafasi hiyo kwa muda ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Ameeleza kuwa uzoefu alioupata katika nafasi mbalimbali ndani ya chama na mwalimu wa vyuo vikuu unampa ujasiri na uwezo wa kusimamia na kutatua kero za wananchi kwa vitendo.

Hata hivyo amesema kuwa tayari amejipima na kujua mahitaji ya wananchi wa Iringa Mjini na nina mpango mahsusi wa kuibua fursa za kiuchumi, kuongeza uwajibikaji wa viongozi na kuboresha huduma za jamii.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii