Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, imemhukumu Shabani Mohamed (27), mkazi wa Mchangani, kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ya kumbaka na kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita. Hukumu hiyo imesomwa Juni 25, 2025 na Hakimu Mkazi Jonas Lyakundi, katika kesi namba 28532/2024, baada ya ushahidi thabiti kuwasilishwa na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mtuhumiwa alitenda makosa hayo Septemba 25, 2024 usiku, baada ya kumvizia mtoto huyo aliyekuwa amelala. Alimbaka na baadaye kumlawiti, kinyume na Kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha Kanuni ya Adhabu [Sura ya 16, Marejeo ya 2022], pamoja na Kifungu cha 154(1)(a) na 154(2) cha sheria hiyo hiyo. Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikamatwa siku hiyo hiyo na kufikishwa mahakamani Oktoba 4, 2024 ambapo alikana mashtaka yote yaliyokuwa yanamkabili.
Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali John Mushi kwa usaidizi wa Mkaguzi wa Polisi Rashid Baleche, uliwasilisha jumla ya mashahidi sita pamoja na vielelezo vitatu mahakamani.
Ushahidi huo uliithibitishia mahakama pasipo shaka yoyote kwamba Shabani Mohamed alitenda uhalifu huo wa kinyama dhidi ya mtoto mdogo, na hivyo kumtia hatiani.