Watoa huduma vituo vya malezi ya wazee wakiri vitendo vya kuwanyanyasa na kuwaonea wazee kwa mwaka 2024

Leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu unyanyasaji dhidi ya wazee ambapo maudhui yam waka huu wa 2025 ni kusaka suluhu ya vitendo hivyo vya unyanyasaji kwenye vituo vinavyotoa huduma ya malezi ya muda mrefu kwa wazee.

Umoja wa Mataifa kupitia wavuti maalum wa siku hii unasema kuwa licha ya kuongezeka kwa hamasa juu ya uwepo wa vitendo hivyo vya ukatili, bado mataifa mengi hayana takwimu za uhakika na zilizochambuliwa kuhusu vitendo hivyo.

Halikadhalika mataifa hayo katika vituo hivyo hakuna watumishi wa kutosha na hata walioko hawana mafunzo ya kutosha ya kulea wazee, jambo linaloweka mazingira ya vitendo vya ukatili na hata wazee kutelekezwa.

Watoa huduma wakiri kuonea wazee

Utafiti ulioungwa mkono na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO ulionesha kuwa takribani asilimia 64 ya watendaji walioko kwenye vituo vya malezi ya wazee walikiri Kutenda vitendo vya ukatili dhidi ya wazee mwaka uliotangulia.

Mambo ya kuzingatia katika hafla hiyo

Ni kwa mantiki hiyo, maadhimisho ya mwaka huu yatajikita kwenye ukatili wanaokumbana nao wazee katika vituo vinavyotoa huduma za malezi yao kwa muda mrefu.

Umoja wa Mataifa umeelaza kuwa ijapokuwa wazee wengi wanaishi kwenye jamii zao, huduma za kwenye vituo vya malezi ni uhalisia kwa wengi.

Wakati huu ambapo mahitaji ya malezi kwenye vituo yakiongezeka kutokana na ongezeko la wazee duniani, vivyo hivyo hofu kuhusu ulinzi wa haki za wazee, usalama wao na utu wao wakiwa kwenye vituo hivyo

Hafla ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wazee duniani

Jumatatu ya tarehe 16 mwezi juni kuanzia saa 7 na dakika 15 kwa saa za Mashariki mwa Marekani kutafanyika mkutano kwa njia ya mtandao kwa takribani saa moja kujadili mustakabali wa huduma za malezi kwa wazee.

Washiriki  kwenye mkutano huo ambapo utamulika mbinu bora pamoja na changamoto zilizopo, na utachangia katika juhudi zenye ushahidi madhubuti za kulinda haki na heshima ya wazee walioko katika vituo vya huduma.

Kwa mujibu wa makadirio ifikapo mwaka 2050, inakadiriwa kuwa mtu 1 kati ya kila watu 6 atakuwa na umri wa miaka 65 au zaidi, jambo linaloongeza hatari ya ukatili dhidi ya wazee.

Takriban mtu 1 kati ya kila watu 6 wenye umri wa miaka 60 na kuendelea walikumbwa na aina fulani ya unyanyasaji katika mazingira ya kijamii katika kipindi cha mwaka uliopita.

Unyanyasaji dhidi ya wazee unaweza kusababisha majeraha makubwa ya mwili na madhara ya kisaikolojia ya muda mrefu.

Unyanyasaji wa wazee unatarajiwa kuongezeka kwani mataifa mengi yanakumbwa na ongezeko la kasi la idadi ya wazee katika jamii zao.

Duniani kote, asilimia 82 ya vifo vilivyokadiriwa kutokana na janga la COVID-19 vilitokea kwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea.

Siku ya kuelimisha umma kuhusu unyanyasaji dhidi ya wazee duniani, tarehe 15 Juni, ilianzishwa na Mtandao wa Kimataifa wa Kuzuia Unyanyasaji kwa Wazee (INPEA) mwaka 2006, na kutambuliwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio  namba A/RES/66/127 lililopitishwa mwaka 2011.

Azimio hilo linazialika nchi wanachama zote, mashirika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa na kikanda, pamoja na jamii ya kiraia, ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi, kuadhimisha siku hii kwa njia inayofaa.

Uvunjaji wa haki za binadamu za wazee ni nini?

Kwa mujibu wa WHO, unyanyasaji kwa wazee unaweza kufafanuliwa kama: "kitendo kimoja au vinavyorudiwa, au kutokuwepo kwa hatua inayofaa, kunakotokea ndani ya uhusiano wa kuaminiana, ambako husababisha madhara au msongo kwa mtu mzee."

Unyanyasaji huu unaweza kuwa wa aina mbalimbali kama vile:

Unyanyasaji wa kimwili

Kisaikolojia au kihisia

Kingono

Kifedha

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii