WAISLAM WA MKOA WA MWANZA WAANDAA DUA MAALUMU

Baraza Kuu la Waislamu Mkoa wa Mwanza limeendesha dua maalum kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na kuliombea Taifa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Dua hiyo imefanyika katika ukumbi wa Gandhi Hall, Jijini Mwanza, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, masheikh pamoja na Waislamu kutoka wilaya zote nane zinazounda Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza na Jembe Habari mara baada ya dua hiyo, baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wamesema kuwa dua hiyo inalenga kuwa kinga kwa taifa, hasa katika kuliepusha na vurugu, migogoro ya kijamii, na kuimarisha mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki nyeti cha uchaguzi.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hasani Kabeke, ameitumia fursa hiyo kuiasa jamii kuwa na utamaduni wa kuliombea taifa hata wakiwa majumbani mwao, badala ya kusubiri wito maalum kutoka kwa viongozi wa dini.

"Dua ni nguzo muhimu katika kutafuta amani na ustawi wa taifa letu. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuwa sehemu ya maombi haya, si lazima tusubiri hadi tuandaliwe ibada maalum," amesema Sheikh Kabeke.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii