Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewapongeza wajumbe wa Kamati
Kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na Makaazi kwa hatua waliyofikia katika
maandalizi ya Sensa ya mwaka huu.
Mhe. Majaliwa ambae pia ni
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na makaazi ameyasema
hayo katika kikao cha tatu cha kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi
wa kambarage jijini Dodoma.
Amesema ni jambo la kupongezwa kwa
hatua iliyofikia sasa katika maandalizi ya Sensa hio inayotarajiwa
kufanyika mwezi Agosti mwaka huu ambapo hatua hiyo inatokana na
mashirikiano yailiyopo baina yao, amesema kuwa ni mategemeo ya Serikali
zoezi hili liweze kufanikiwa vizuri zaidi.
Mhe. Majaliwa ametaka
wajumbe hao kuhakikisha wanaendeleza kushirikiana kwa pande zote za
Muungano jambo ambalo litasaidia kufanikisha zoezi hilo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti mwenza wa kamati hio kitaifa ambae pia ni Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdalla amesema kuwa
hatua iliofikiwa hadi sasa katika maandalizi ya Sensa hio ni jitihada za
Marais wote wawili, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hasan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dkt Husein Ali Mwinyi wanazoendelea kuzichukua katika kufanikisha
zoezi hilo
Aidha, Mhe. Hemed amewataka wajumbe wa kamati hio
kuhakikisha kuwa wanasimamia vyema majukumu yao ili Sensa hii iweze
kufikia lengo la Serikali zote mbili kuweza kupanga mipango Imara ya
kimaendeleo kwa maslahi ya Taifa
Sambamba na hayo, Mhe.Hemed
amesema Serikali zote mbili zimejipanga kuhakikisha zoezi hilo
linafanikiwa na linakamilika kwa wakati uliopangwa kwani Sensa ya mwaka
huu ni ya kipekee ambayo itaibua mambo mbali mbali yatakayozisaidia
Serikali zote katika kuwaletea Maendeleo wananchi wake.
Nae
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Ndugu JOHN
JINGU amesema kuwa jitihada mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa kwa
kuelimisha jamii kuhusu suala zima la Sensa na kueleza kuwa hadi sasa
tayari wameshayafikia makundi ya wananchi tofauti kwa semina nakutumia
vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu ya Sensa inamfikia kila mmoja
katika jamii.
Kwa upande wake, mtakwimu mkuu wa Serikali wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. ALBINA CHUWA amesema mashirika ya
ndani na nje ya nchi tayari wameshaonesha ushirikiano wao ili
kuhakikisha zoezi hilo linakamilika bila ya changamoto yoyote. Aidha,
amesema Ofisi zote mbili za takwimu zimejipanga kuhakikisha makarani
watakao kusanya taarifa wanatoka katika maeneo husika ili kupata taarifa
za usahihi.