Kesi ya CHADEMA yapigwa kalenda hadi Julai 10

Kesi iliyofunguliwa na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kutoka Zanzibar, imepangwa kusikilizwa Julai 10 mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Wajumbe hao ni aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Walifungua kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA wakidai kwamba Chama hicho, kimekuwa kikiitenga Zanzibar katika kuendesha shughuli zake ikiwemo suala la rasmali fedha.

Kesi hiyo ilishindwa kuanza kusikilizwa leo mbele ya Jaji Hamidu Mwanga, ambapo iliahirishwa mbele ya Msajili Aziza Mbage kwa taarifa kwamba jaji hayupo anasikiliza kesi nyingine Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara. Kutokana na hali hiyo, kesi iliahirishwa hadi Julai 10, 2025.

Awali, wajumbe hao waliomba zuio la muda hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,  Juni 10, 2025 Mahakama iliwakubaliwa ombi hilo kwa kutoa zuio la muda kwa CHADEMA kutokufanya shughuli zozote zile za kichama hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Pia, Mahakama hiyo imemzuia Katibu Mkuu, mawakala na wafuasi wa chama hicho ambao wamepewa dhamana ya kuendesha shughuli za chama kutokushiriki kwa namna yoyote kwenye shughuli za kisiasa hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa.

Hata hivyo iliagiza mali zote za CHADEMA zisitumike hadi kesi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii