Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeiagiza
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kufanya uchunguzi wa nauli zinazotozwa
na mashirika washindani katika safari za ndani, na kuweka nauli ambazo
zitawavutia Watanzania wengi zaidi kutumia ndege zao.
Agizo hilo
limetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya
wakati akijibu swali la Mbunge wa Gando, Salim Mussa Omari aliyetaka
kujua nini kinasababisha mabadiliko makubwa ya bei za tiketi za ATCL kwa
safari za Dar es Salaam na Dodoma ambapo mara nyingi hufika hadi
shilingi laki sita.
Naibu Waziri ameeleza kwamba uuzaji wa tiketi
katika biashara ya usafiri wa anga ni moja ya mikakati ya ushindani ili
kuvutia wateja ambapo tiketi hupangwa kwa ngazi mbalimbali kizingatia
vigezo kama bei ya tiketi, ujazo wa ndege, muda wa kukata tiketi
masharti ya tiketi na daraja la tiketi.
“Mteja ambaye anataka
tiketi mapema na kukuta ndege haijajaa, hupata tiketi kwa bei ya chini,
ikilinganishwa na mteja anayekata tiketi yake muda mfupi kabla ya safari
na kukuta ndege imejaa, hupata bei ya juu,” ameeleza.
Kasekenya
amesema kwa safari za Dar es Salaam na Dodoma, kwenda na kurudi, ATCL
ina ngazi 13 katika daraja la kawaida (economy class) ambapo bei zake
zinaanza shilingi 331,400 hadi 678,400. Ameongeza kuwa kuna kuna daraja
la biashara (business class) ambalo lina ngazi tatu zenye huduma maalum
na nauli zake ni kati ya shilingi 721,600 hadi 953,000.
Licha ya maelezo hayo, ATCL imeagizwa kufanya mapitio na kupanga nauli zinazoweza kuwavutia Watanzania kutumia ndege hizo.