IKIWA imebaki miezi minne kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu hekaheka na sarakasi za watia nia zimeshika kasi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo mbalimbali nchini.
lina taarifa kuwa katika majimbo mengi nchini wabunge wa sasa wananyukana na watia nia wapya huku katika majimbo yaliyogawanywa wabunge wakikimbia ngome zao kwa hofu ya kuadhibiwa na wananchi na wengine kuwahofia watia nia wapya.
Vilevile katika majimbo mengine inadaiwa watia nia wapya na wabunge wa majimbo husika wamekuwa wakishindana kwenye kutoa misaada kwa wananchi kwenye maeneo ya ada za shule, afya, misiba kwa kupeleka chakula, michezo na hata kufadhili vikao mbalimbali.
Mkoa wa Dar es Salaam
Miongoni mwa majimbo yanayoonekana kuwa na ushindani ni Temeke ambapo kunatajwa watia nia Mbunge wa sasa Doroth Kilavi, mwanahabari Shafi Dauda, Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, Mariam Kisangi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Tano Mwera na Diwani wa Keko, Jasdeep Babhra.
Mkoa wa Katavi
Katika Jimbo la Tanganyika ambalo zamani lilikuwa Mpanda Vijijini mkoani Katavi, mnyukano unatajwa kuwa ni kati ya mbunge wa sasa Selemani Kakoso akichuana na mtia nia mpya, William Makufwe.
Mkoa wa Simiyu
Jimbo la Bariadi Vijijini limetikiswa na vigogo wawili ambao ni mbunge wa sasa na Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.
Mbunge huyo ambaye aliahidi kutetea kiti chake kupitia Jimbo la Bariadi Vijijini alilazimika kubadili gia angani baada ya kutokea kwa mnyukano kati yake na Kadogosa.
Wakati akijipanga kuwania ubunge kupitia jimbo hilo, upande wa pili Kadogosa naye alikuwa akijipanga kutafuta tiketi ya kwenda bungeni kupitia jimbo hilo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alithibitisha kuwa kutokana na hali hiyo ameamua kubadilisha uamuzi wake na sasa atakwenda kugombea Jimbo la Bariadi Mjini, lengo likiwa kukinusuru chama kisigawanyike kwani mvutano uliokuwepo baina ya wafuasi wao ulikuwa mkubwa, ambao ungekiacha chama katika hali mbaya hata kufikia kulipoteza jimbo.
Mnyukano sasa umehamia katika Jimbo la Bariadi Mjini kutokana na maamuzi ya Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Simiyu, Lucy Sabu ambaye sasa atatifuana na Kundo Mathew.
Lucy alitangaza nia hiyo akiwa Jijini Dodoma, akibainisha kuwa amejitafakari na kuona anao uwezo mkubwa na nia ya kuweza kugombea jimbo hilo na kuwatumikia wananchi wake.
Mkoa wa Kigoma
Katika Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Mbunge wa sasa, Felix Kavejuru anakabiliwa na upinzani mkali ndani ya CCM kwa sababu hadi sasa wanachama 14 wameonesha nia ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge kwenye jimbo hilo.
Baadhi ya watia nia waliojitokeza na kutangaza hadharani ni pamoja na Profesa Pius Yanda, Ellias Kayandabhila, Cassian Mbajije, Amos Dyegula, mmiliki wa Standard FM ya Singida, James Daud ambao wanaelezwa kusubiri kuanza mchakato wa uchuakuaji fomu Juni 28, mwaka huu.
Kwa upande wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mbunge wa jimbo hilo, Kirumbe Ng’enda anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Msanii na Mtangazaji wa Wasafi FM, Clayton Revocatus ‘Baba Levo’ na Baruani Muhuza wa Azam Media.
Katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Mbunge anayemaliza muda wake, Assa Makanika anakabiliwa na upinzani katika kutetea kiti chake kutoka kwa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Peter Serukamba.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Evance Chocha maarufu kama Dubai sambamba na aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo, Daniel Nsanzugwanko.
Katika Jimbo la Muhambwe, Dk Florence Samizi naye pia yupo kwenye wakati mgumu kutokana na kukabiliwa na upinzani kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Jamal Tamim.
Mkoa wa Arusha
Mkoani Arusha joto la kisiasa limepanda katika mkoa huo hususani katika Jimbo la Arusha Mjini ambalo anahusishwa kulitaka kwa udi na uvumba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda huku mwenye jimbo lake, Mrisho Gambo akionesha nia ya kutaka kuendelea kuwatumikia wananchi wa Arusha Mjini.
Juzi Makonda akiwa Jijini Arusha wakati wa kuvunja Baraza la Madiwani alisikika akisema kuwa wamuombee na pale wakisikia jina lake huko nje linatajwatajwa wamuunge mkono.
Mbali na hao, mwana CCM mwingine ambaye anatajwa kuwania nafasi hiyo ni Justin Nyari ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite ambaye aliwahi kuwania nafasi hiyo mwaka 2015 na kushika nafasi ya pili nyuma ya mfanyabiashara wa Nafaka, Phillemon Mollel.
Katika Jimbo la Longido wana CCM watatu wameonesha nia ya wazi kuwania nafasi ya ubunge ambayo inashikiliwa na Mbunge wa sasa na Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa.
Wanachama hao ni pamoja na wakili wa kujitegemea, Nicolaus Seniteu, Petro Oltukai na Kaimu Katibu Tarafa wa Ketumbein, Joseph Kulunju.
Kwa upande wa Jimbo la Ngorongoro wana CCM wanane wameonesha nia ya kuwania nafasi ya ubunge inayoshikiliwa kwa sasa na Emmanuel Shangai.
Wanachama hao ni Profesa Kokel Melubo, Elizabert Sinodya, Rose Njilo, Joseph Parsambei, Valentin Ngorisa, Patrick Ngwediai, Kamaoni Kalambani na Yanik Ndoinyo.
Katika Jimbo la Karatu mbunge wa sasa, Daniel Awack anakabiliwa na upinzani kutoka kwa wanachama wanane wa CCM ambao ni Mwalimu Pantaleo Paresso, Patrick Chele, Secilia Pareso na Balozi Patrick Nsele ambaye aliwahi kuwania nafasi hiyo mwaka 2020.
Kwa upande wa Jimbo la Arumeru Mashariki, watia nia wawili vijana na wenye ushawishi mkubwa wanatarajiwa kumpa wakati mgumu mbunge wa sasa, John Palangyo.
Wanachama hao ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Joshua Nassari na Katibu Mwenezi wa CCM wa jimbo hilo, Kennedy Mpumilwa.
Ndani ya Jimbo la Arumeru Magharibi mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya Mbunge wa sasa, Noah Seputu dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, Elias Lukumay, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Noel Severe na Dk Johannes Lukumay.
Mbunge wa Monduli, Fred Lowassa anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Joseph Isack maarufu kwa jina la kadogoo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengema, Mkuu wa zamani wa Mkoa wa Morogoro, Loota Sanare na aliyewahi kuwa katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Daniel Parokwa.
Mkoa wa Mbeya
Katika Jimbo la Mbeya Mjini linaongozwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliyekwisha kutangaza kuhamia Jimbo la Uyole kutokana na mgawanyo wa jimbo hilo, makada saba wanatajwa kuwania nafasi hiyo huku baadhi yao wameshaweka wazi nia yao.
Miongoni mwao ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Patrick Mwalunenge, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Afrey Nsomba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa (NEC), Ndele Mwaselela.
Wengine ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu mkoani humo, Dk Mary Mwanjelwa, mjumbe wa mkutano mkuu taifa, Charles Mwakipesile pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa huo, Dk Stephen Mwakajumilo.
Kwa upande wa Jimbo la Rungwe makada watano wamejitokeza kulitaka ambao ni mbunge wa sasa, Antony Mwantona, Dk Samuel Mafwega, Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda na Aliko Mwaiteleke.
Mkoa wa Iringa
Kadiri siku zinavyosogea kuelekea Uchaguzi Mkuu majina kadhaa yanatajwa katika Jimbo la Iringa Mjini huku Mbunge wa sasa Jesca Msavatavangu likiwa miongoni mwao.
Wanasiasa wengine wanaotarajiwa kumpa wakati mgumu katika uchaguzi wa ndani wa CCM ni Fadhili Ngajilo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Iringa, naye ametangaza wazi nia ya kuwania ubunge jimbo hilo.
Wengine ni Wakili Moses Ambwindwile, Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, ambaye anapewa nafasi kutokana na ukaribu wake na uzoefu wa kusimamia miradi ya maendeleo ya halmashauri.
Majina mengine yanayosikika ni pamoja na Nguvu Chengula, Islam Huwel ambaye anabebwa na uzoefu wake katika sekta binafsi na Peter Msigwa.
Mkoa wa Pwani
Mtifuano mkubwa unatajwa katika Jimbo la Kibaha Mjini ambapo Mbunge wake, Silvestry Koka atakumbana na Abubakar Alawi wakati wa kutafuta mgombea ubunge wa jimbo hilo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.