WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na taasisi nyingine za elimu, kusimamia na kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa kuanzia elimu ya msingi mpaka elimu ya juu ili kuendelea kukidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Majaliwa alisema hayo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho ya Miaka 20 ya Chuo Kikuu cha Waislamu (MUM) mkoani Morogoro.
Pia, amezitaka taasisi za elimu nchini ziimarishe mahusiano na vyuo vyote nchini vinavyotoa maarifa kwa vijana wa Kitanzania pamoja na kuzalisha wakufunzi ili kuwa sehemu ya mtandao wa utoaji maarifa na taaluma yenye ubora wa hali ya huu.
Alisema serikali inaendelea na ujenzi wa Mfumo wa Takwimu wa Sekta ya Elimu utakaowezesha upatikanaji wa takwimu zote za sekta hiyo ambao utakuwa na uwezo wa kupokea takwimu zinazohusiana na elimu kutoka katika mifumo mingine ya serikali ikiwamo Nida, Rita na Wizara ya Mambo ya Nje.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika kuunga mkono jitihada za wadau kuchangia maendeleo ya chuo hicho kupitia mfumo maalumu, Rais Samia ametoa Sh milioni 100 ili kiendelee kutoa huduma kwa watoto wa Kitanzania.
Aliongeza kuwa wamefikia mfano katika fedha tujenge madarasa ya kutosha tujenge mabweni hapa na kadhalika na mimi nikiwa hapa nataka nikuunge mkono Profesa kwenye mchango wetu na ninatoa Shilingi milioni 10 na pia, Rais ametoa Shilingi milioni 100”.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga alisema katika kipindi cha miaka 20, chuo hicho kimekuwa na programu zaidi ya 32 kutoka programu mbili wakati kinaanza na kimetoa wahitimu zaidi ya 15,000.
Alisema Mum imeweka mipango inayozingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na mwelekeo mpya wa elimu Tanzania unaolenga kutoa elimu ujuzi, stadi na maarifa ili kuwajengea wahitimu uwezo na sifa za kujiajiri na kujiajiri katika soko shindani la ajira duniani.
Naye Makamu Mkuu wa chuo kikuu hicho, Profesa Mussa Assad alisema moja ya changamoto kubwa kukosekana kwa hosteli za wanafunzi wa kike.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Waislamu (MDF), Dk Ramadhani Dau alisema bodi na uongozi wa chuo wanamshukuru Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa uamuzi wa kuwakabidhi majengo yaliyokuwa Chuo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mwaka 2005 ili kuanzisha chuo kikuu hicho.
Dk Dau alisema mwaka huo walianza na wanafunzi 167, lakini hadi kinatimiza miaka 20 kina wanafunzi zaidi ya 5,000 Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir alihimiza mikakati ya kusaidia chuo kiendelee kufanya vizuri.