Marobota ya Pamba yanayonunuliwa ndani ya nchi kutotozwa VAT

SERIKALI imesema marobota yote ya pamba yatakayonunuliwa kutoka kwa wakulima na kuuzwa ndani ya nchi hayatatozwa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuanzia sasa tofauti na ilivyozoeleka awali.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kuongeza kuwa kwa kawaida marobota ya pamba yanayotozwa kodi ni yake yanayouzwa hapa nchini na yanayoenda nje ya nchi hayatozwi kodi.

Aidha, alisema ili kukuza uzalishaji wa pamba, serikali imepanga kuanza uzalishaji wa mbolea maalumu kwa ajili ya zao la pamba na kwamba mbolea hiyo nayo itatolewa kwa ruzuku kama mbolea nyingine ili kuwawezesha wakulima wote wa pamba kumudu gharama zake.

Alisema kutokana na mipango ya serikali kuinua zao la pamba, katika miaka mitatu iliyopita kiwango cha pamba iliyozalishwa haizidi tani 60,000 wakati mwaka huu pekee serikali inatarajia kuvuna kuanzia tani 200,000 hadi 270,000 kwa Mkoa wa Simiyu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda alisema serikali imedhamiria kuwafanya vijana wa Simiyu kumudu kujiajiri kwa kuwapelekea vyuo vya ufundi vya Veta katika wilaya za Bariadi, Maswa, Busega na Meatu.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema juhudi za Rais Samia kuimarisha sekta ya afya zimewafanya wanawake wa Simiyu kuwa na afya nzuri, hali inayowafanya waume zao kuwatunza vizuri na kusababisha asilimia ya uzazi mkoani humo kuwa juu.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema ajenda ya taifa ya kuvuna na kutumia maji ya Ziwa Victoria imetekelezwa kwa vitendo na Rais Samia kwa kuwawezesha wananchi wa Simiyu nao kuwa na uhakika wa kuyapata.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii