RAIS Samia Suluhu Hassan amesema ujio wa shule za amali pamoja na ufundi zenye michepuo ya ufundi, kilimo, muziki na fani mbalimbali unakwenda kutatua changamoto ya ajira hasa kwa vijana.
Alisema serikali imeamua kubadilisha mwelekezo wa elimu nchini kwa kuanzisa shule hizo ambazo lengo lake kubwa ni kuhakikisha mtoto akihitimu elimu ya sekondari awe na ujuzi pamoja na uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri.
Rais Samia alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mwamapalala Amali iliyoko katika Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku tano mkoani humo.
Uwekaji jiwe la msingi shule hiyo uliendana sambamba na shule nyingine 26 ambazo zinajengwa na serikali katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara.
Alisema mwelekeo wa serikali ni kukuza zaidi elimu ya amali na ufundi kutokana na elimu iliyopo kwa sasa kutomwezesha mtoto ambaye anahitimu elimu ya sekondari kukosa ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.
Rais Samia aliwataka wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa shule hizo zote 26 kuhakikisha wanaongeza kasi ya ujenzi na wakamilishe kwa wakati, ili wanafunzi kuanza masomo yao ifikapo Januari mwakani.
Aliwataka wazazi kutumia nafasi hii kuwapeleka vijana wao katika shule hizo kwani serikali inatumia gharama kubwa katika kuboresha sekta ya elimu ya msingi, sekondari, ufundi pamoja na amali ikiwemo vyuo.
Awali, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema ujenzi wa shule 26 unaendelea na upo katika hatua za mwisho za kukamilika ili shule zote zianze kufanya kazi Januari 2026.
Alisema hatua ya ujenzi wa shule hizo ni maagizo ya Rais Samia katika kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ambapo mageuzi hayo ni kujenga shule hizo za amali na ufundi, ambazo awali zilikuwepo lakini zinafifia.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEM), Mohamed Mchengerwa alisema Sh bilioni 41.6 kinatumika katika kujenga shule zote 26 na katika Shule ya Mwamapalala Itilima ujenzi wake unagharimu Sh bilioni 1.6.