Kada wa Chama cha ACT-Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema katika uchaguzi wa mwaka huu hawamtumi mtoto, badala yake wanaenda wenyewe kwa ajili ya kusimamia haki na kuhakikisha mshindi halali anatangazwa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Bakhresa, Manzese jijini Dar es Salaam, Sheikh Ponda alisema kuwa atakuwa mstari wa mbele katika uchaguzi huu, akisisitiza kuwa ana uzoefu wa kutosha kutokana na kushiriki siasa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Amesema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, mafanikio ya vyama vya upinzani yalitokana na utoaji wa elimu ya uraia kwa wananchi kuhusu hali halisi ya siasa nchini, pamoja na ulinzi wa kura na msimamo wa raia waliotaka kuona haki ikitendeka.
Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, matokeo hayo mazuri yaliwezesha vyama vya upinzani kupata zaidi ya wabunge 40 na madiwani zaidi ya 900 kote nchini.
Amebainisha kuwa baadhi ya wagombea wa upinzani waliotangazwa washindi katika kipindi hicho walisaidiwa na nguvu ya wananchi waliotetea matokeo, akiwataja Halima Mdee wa Jimbo la Kawe na Godbless Lema wa Jimbo la Arusha Mjini kuwa ni miongoni mwao.
Amesema siasa si jambo jipya kwake kwani ameshiriki kuandaa vyama, sera na kuwaandaa vijana kushiriki katika harakati za kisiasa. Alisisitiza kuwa: “Huko nyuma kama mlikuwa mnasikia mslogan Yale Ngangari, ndiyo sisi.”
Sheikh Ponda ameongeza kuwa mapambano ya kisiasa hayawezi kufanikiwa nje ya nchi, bali ni lazima kufanywa ndani kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli.