Serikali yawekeza Tsh. bilioni 1 kununua vifaa tiba halmashauri ya mji wa Handeni

SERIKALI imewekeza ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vya Sh bilioni 1 kwenye sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji Handeni na kuimarisha huduma za afya.

Uwekezaji huo ni pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika halmashauri hiyo kwa kipindi cha miakaminne (2021–2024).

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni, Dk Hudi Shehdadi amesema baadhi ya vifaa tiba vilivyonunuliwa ni mashine ya Digital X-Ray, mashine ya Ultrasound, Dental Chair, Dental X-Ray, mashine ya usingizi (anesthesia machine), na kabati la kuhifadhia maiti (mortuary cabinet).

Vifaa vingine vilivyopokelewa ni mashine ya kuchoma taka hatarishi ya kisasa (hi-tech incinerator), mashine za kufulia nguo, majokofu ya kuhifadhia damu salama, gari la kubebea wagonjwa (ambulance), gari la usimamizi wa huduma za afya, na mfumo wa kusambaza gesi ya oksijeni kwa wagonjwa.

Dk Shekhidadi amesema kuwa uwekezaji huo umeongeza ufanisi na ubora wa huduma, na hivyo kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za nje ya wilaya.

Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha ustawi wa wananchi kupitia huduma bora za afya.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii