Umoja wa Afrika kuthamini maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania utakaofanyika Oktoba 2025

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amekutana na Misheni Maalum ya Umoja wa Afrika ya Kutathmini Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, na kuahidi kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa haki, uhuru na amani.

Misheni hiyo ya tathmini kabla ya uchaguzi (Pre-election Assessment Mission – PAM), iliyoongozwa na Dk. Phumzile Mlambo-Ngcuka, Makamu wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, iliwakilishwa na wajumbe 16, na ilifanya mazungumzo na Waziri Mkuu jana Juni 17, 2025 katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Phumzile alisema kuwa Misheni hiyo imeridhishwa na maandalizi ya uchaguzi yanayoendelea nchini, ikiwemo mazingira ya kisiasa na mabadiliko ya sera na mifumo yaliyoanzishwa na Serikali kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi.

Tumefurahishwa pia kuona kuna idadi kubwa ya wadau wa siasa nchini na mageuzi makubwa yaliyofanyika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi .

Aidha alisisitiza kuwa Misheni hiyo imetiwa moyo na kiwango cha juu cha ushiriki wa wanawake katika siasa, hatua aliyosema inaashiria mwelekeo wa kufikia usawa wa kijinsia kwenye uongozi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii