Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia Ofisa wa jeshi la Magereza mwenye cheo cha Sajini aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Nyange kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Rauya iliyopo wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro
Kwa mujibu wa Taarifa ya jeshi la polisi iliyotolewa na kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ,kamishna msaidizi wa Polisi (ACP )Abel Mtagwa,tukio Hilo limetokea Juni 14 mwaka huu saa kumi jioni kwenye Kitongoji cha Mrokora Kijiji cha Rauya kata ya Marangu Mashariki.
Kamanda Mtagwa amesema mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 13,alibainika kulawitiwa na askari huyo wa jeshi la magereza ambaye kituo chake cha Kazi ni gereza kuu la mkoa wa Kilimanjaro la Karanga.
Kamanda Mtagwa amesema hadi Sasa askari huyo anashikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi mji mdogo wa Himo huku taratibu za kiutumishi za kijeshi zikiendelea na baada ya taratibu hizo kukamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.