Rufaa dhidi ya adhabu ya kifungo cha maisha gerezani iliyotolewa kwa washtakiwa wanne waliokutwa na hatia kwenye kosa la kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti Mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la X itaanza kusikilizwa kesho Juni
3, 2025.
Wakata Rufaa katika kesi hiyo ni aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo, Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Wakata rufaa hao walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani Septemba 30, 2024 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti Mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam kwenye mahakama iliyoendeshwa kwa faragha.
Mbali na kifungo hicho cha maisha warufani hao pia walitakiwa kumlipa binti huyo kiasi cha Sh1 milioni kila mmoja kutokana na majeraha waliyomsababishia.
Akizungumza na Mwananchi Wakili wa warufani hao Godfrey Wasonga amesema taratibu zote za kukata rufaa zimeshakamilika na kesi hiyo itaanza kusikilizwa kesho Juni 3, 2025 Mahakama Kuu ya Dodoma mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa Amir Mruma.