Agizo la Rais Samia Suluhu la kumtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda kamati kuchunguza matukio ya mauaji mkoani Mtwara na Kilindi, Tanga limewaibua ndugu wa askari mwingine, Linus Mzema aliyeuawa kwa risasi na polisi wenzake Mwanga mkoani Kilimanjaro Mei 2021.
Ndugu hao wameibuka baada ya kuguswa na maelekezo ya Rais Samia aliyoyatoa Ijumaa iliyopita akiwa njiani kwenda mkoani Mara, akisema “haiwezekani polisi wahusishwe na mauaji halafu wajichunguze wenyewe.”
Lucia Mkepule ambaye ni mama mzazi wa askari Linus Nzema na Atilio Kalinga ambaye ni mjomba wa marehemu, wameomba kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu ichunguze pia mauaji ya Mwanga kwa kuwa hakuna askari polisi aliyeshtakiwa mpaka sasa.
“Rais Samia ni mama kama mimi na naamini ana uchungu na mtoto. Ile kamati iliyoundwa kwa maagizo yake iende Kilimanjaro, ili haki itendeke,” alidai Lucia alipozungumza na Mwananchi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema jalada la shauri hilo lilikwenda kwa DPP na ikaonekana hapakuwa na jinai na lilishamalizwa kijeshi.
Kauli ya Rais Samia iliyowaibua wazazi wa askari huyo, ilitokana na taarifa ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis (25) ambaye inadaiwa baada ya mauaji yake, mwili wake ulitupwa baharini hadi upelelezi makini ulipobaini ukweli.
Rais alitoa agizo hilo wakati maofisa saba wa jeshi hilo waliotuhumiwa kwa mauaji ya Mtwara wakiwa wamefikishwa kortini kuhusiana na mauaji hayo, huku mmoja kati yao, mkaguzi msaidizi Grayson Mahembe akidaiwa kujinyonga akiwa mahabusu mkoani humo.
Kutokana na agizo la Rais Samia, tayari Waziri Mkuu ameunda kamati ya kuchunguza tukio hilo, huku akiagiza kusimamishwa kazi kwa Kamanda wa Polisi (RPC) mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Upelelezi (RCO) wa mkoa huo na mkuu wa kituo (OCS) cha Mtwara Mjini ili kupisha uchunguzi.
Kamati hiyo pia inachunguza mauaji ya watu sita waliouawa wilayani Kilindi katika kinachoelezwa ni ugomvi wa wakulima na wafugaji.
Hatua hizo ya Rais Samia zimeibua tukio la askari polisi Mzema aliyeuawa kwa kupigwa risasi ya shingo na askari mwenzake Mei 31, 2021 katika Kijiji cha Ndafu Wilaya ya Mwanga, kisha polisi wakadaiwa kubadili taarifa ya sababu ya kifo na kueleza kilitokana na kugongwa na pikipiki.
Hata hivyo, Mwananchi lilifanya uchunguzi wa kina na kupata watu walioshuhudia tukio hilo kuwa walimuona mmoja wa polisi akichukua bunduki kwenye gari lao kutoka kiti cha mbele kwa dereva na kumfyatulia mwenzake.
Baada ya ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai nchini (DCI) aliunda timu kuchunguza tukio hilo na kubaini kuwa Mzema hakufa kwa ajali, bali aliuawa kwa kupigwa risasi ya bunduki mali ya Jeshi la Polisi nchini.
Katika eneo la tukio la mauaji ya polisi huyo, kulipatikana damu za marehemu na gololi tano za bunduki aina ya shortgun na uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa siku ya tukio, polisi waliokuwa doria walikuwa na silaha za aina hiyo pia.
Lakini taarifa nyingine zilidai wakati Nzema anafikishwa Kituo cha Afya Kileo alikuwa tayari amefariki na polisi waliompeleka hapo walimwagiza muuguzi kushona jeraha lililokuwa shingoni ambalo risasi ziliingilia.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, katika gololi sita za shotgun ilikuwa inakosekana moja na ndiyo ilipatikana Juni 20, 2021 baada ya mwili wa polisi huyo kufukuliwa katika Kijiji cha Kibete, Mufindi ulipozikwa na kuchunguzwa upya.
Askari polisi tisa walishikiliwa na Polisi kwa zaidi ya siku zaidi 50 kuhusu tukio hilo, lakini waliachiliwa Agosti 24, 2021 bila taarifa yoyote.
Nae,Mama mzazi wa Mzema, Lucia Mkepule alidai tangu tukio hilo hajui chochote kinachoendelea.
“Tumepata shida sisi tunakimbilia polisi, lakini hiki kinachofanyika ndani ya polisi mimi kujua ameuawa kwa risasi na askari mwenzie na walikamatwa baadae wakaachiwa. Mpaka sasa hakuna kesi yoyote mahakamani.
“Niliwahi kupata karatasi zinazosema eti alikufa kwa ajali ya pikipiki. Ni za uongo. Nilitaka niende kituo chake cha kazi niwaulize, hivi kweli mnathibitisha hili na mmekaa kimya kana kwamba aliyeuawa ni mbwa?” alihoji mama huyo.
Lucia aliomba kilio chake kimfikie Rais Samia, ili haki itendeke.
“Nilivyofanya utafiti inaoneokana polisi wenzake waliandaa wamtupe mahali, ili aonekane amekufa kwa kifo kingine, tu kwa sababu yule mtoto hakuwa zamu siku anakufa. Alifuatwa nyumbani.”
“Mmoja alimtafuta kwa njia ya simu akawaambia mie najisikia vibaya, mmoja akamfuata mpaka nyumbani akawaongezee nguvu. Ndio maana nataka haki itendeke kwa sababu wale wenzake wako kazini ingawa wamebadilishwa vituo,” alilalamika Lucia.
Alidai kuwa hata mazishi yake hayakuwa katika mazingira rafiki.
“Walifika na ule mwili saa 12 kasoro. Nilivyodai kumuona hawakuniruhusu hadi nilipochachamaa. Nilipolazimisha na kumgusa nikaona ana jeraha hapa shingoni.
Mjomba wa marehemu, Atilio Kalinga alimuomba Rais kuingilia kati suala hilo kama alivyofanya la Mtwara, ili waliohusika na tukio hilo washtakiwe.