Marekani imetangaza kuwa itaanza kufuta viza za Wanafunzi kutoka China hususani wale wanaohusishwa na Chama cha Kikomunisti cha China au wanaosomea fani zinazotajwa kuwa nyeti kwa usalama wa Taifa.
Tangazo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio siku ya jana ambaye pia amesema kuwa masharti ya viza yatapitiwa upya ili kuongeza uchunguzi kwa maombi kutoka China na Hong Kong.
Ikiwa tangazo hilo limekuja siku moja baada ya kuripotiwa kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesitisha kwa muda miradi mipya kwa Wanafunzi na waombaji wa viza za kubadilishana Wanafunzi hao.
Mpango huo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za utawala wa Rais Donald Trump za kuimarisha udhibiti wa uhamiaji, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchunguzi wa mitandao ya kijamii kwa Wanafunzi wa kimataifa kwa kufuta viza na kuharakisha hatua za kuwarejesha makwao.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Elimu ya Kimataifa (IIE) China ilikuwa na idadi ya pili kwa ukubwa ya Wanafunzi wa kimataifa waliokuwa wakisomea Marekani mwaka 2023/2024, wakiwa 277,398, hadi sasa Ubalozi wa China nchini Marekani haujatoa kauli rasmi kuhusiana na tangazo hilo, Wachambuzi wanasema hatua hii huenda ikaathiri uhusiano wa kielimu na kidiplomasia kati ya Mataifa hayo mawili yenye mvutano wa muda mrefu.