Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani umeyataka mashirika ya Serikali kufuta mikataba na Chuo Kikuu cha Harvard yenye thamani ya kiasi cha dola milioni 100.
Hatua hiyo ya Trump ni sehemu ya mapambano dhidi ya chuo hicho kikongwe na tajiri zaidi nchini Marekani.
Uamuzi huo wa jana unakuja wakati tayari utawala wa Trump ukiwa umeshafuta ruzuku ya zaidi ya dola bilioni 2.6 kwa taasisi hiyo ya elimu, ambayo imekataa kufuata matakwa ya utawala huo yanayoitaka kubadilisha sera zake kadhaa.
Trump anadai kuwa chuo kikuu hicho ni kituo cha uzalishaji wa fikra za kiliberali na chuki dhidi ya Mayahudi.
Hata hivyo wakosoaji wengi wa Trump wanaona kuwa kiongozi huyo anatumia kisingizio hicho kuimarisha nafasi yake miongoni mwa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia.