Wanajeshi waliotumwa Los Angeles watarejesha 'utulivu,' asema Trump

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza Jumapili, Juni 8, kwamba askari wa kikosi cha walinzi wa taifa aliowatuma Los Angeles kinyume na matakwa ya mamlaka ya jimbo hilo kushughulikia maandamano dhidi ya sera yake ya uhamiaji watarejesha "utulivu." 

Kutumwa kwao kunakuja katika siku ya tatu ya maandamano yaliyokumbwa na makabilianono na vurugu katika jiji kuu la California, ambako wanaishi watu wengi kutoka jamii kubwa ya Wahispania, wakati wakaazi walijaribu kupinga kukamatwa kwa wahamiaji kwa nguvu kulikofanywa na mamlaka ya Uhamiaji ya Shirikisho (ICE).

"Mna watu wenye jeuri wanaochochea vurugu, na hatutawaacha waondoke," amewaambia waandishi wa habari. "Tutarejesha  utulivu," ameahidi, pia akisema anafikiria kutuma wanajeshi mahali pengine. "Hatutaruhusu jambo la aina hii kutokea kwa nchi yetu."

"Tutarejesha utulivu," ameongeza rais huyo kutoka chma cha Republican, akisema amekuwa akifuatilia hali hiyo "kwa karibu sana." Ameongeza kuwa hajasita kutuma wanajeshi kwingineko nchini Marekani ikibidi. "Hatutaruhusu jambo la aina hii kutokea kwa nchi yetu," amesema. "Tukiona hatari kwa nchi yetu na raia wetu, tutakuwa thabiti sana katika kutekeleza sheria na kudumisha utulivu," amebainisha. 

"Matumizi mabaya ya kutisha ya madaraka," amelaani magavana wa California kutoka chama cha Democratic

Kulingana na Kenneth Roth, mkuu wa zamani wa shirika lisilo la kiserikali la Human Rights Watch, hii itakuwa mara ya kwanza tangu mwaka 1965 kwa rais kupeleka wanajeshi hao bila ombi la awali kutoka kwa gavana wa jimbo.

Magavana wa chama cha Democratic nchini Marekani wameshutumu "utumiaji mbaya wa madaraka" uliofanywa na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alituma wanajeshi 2,000 wa kikosi cha walinzi wa taifa huko Los Angeles, kinyume na matakwa ya Gavana wa California kutoka chama cha Democratic, Gavin Newsom. "Uamuzi wa rais Trump kupeleka wanajeshi wa kikosi cha walinzi wa taifa huko California ni matumizi mabaya ya kutisha ya madaraka," magavana walisema katika taarifa ya pamoja. “Ni muhimu tuheshimu mamlaka kuu ya magavana wa taifa letu kusimamia wanajeshi wa kikosi cha walinzi wao wa taifa,” wameongeza, wakisisitiza uungwaji mkono wao kwa Gavin Newsom.

Gavana wa California alipinga hatua hiyo, akiiita "uchochezi wa kimakusudi" na kudai kwamba "itaongeza tu mivutano." "Nilimpigia simu hivi majuzi usiku. Nikasema, 'angalia, unapaswa kulishughulikia hili. Vinginevyo, ninatuma askari.' Na ndivyo tulivyofanya," rais Donald Trump amesema Jumapili. Onyo ambalo amefuata tangu wakati huo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii