Edgar Lungu alizaliwa Novemba 11,1956 katika mji wa Ndola mkoa wa viwanda wa Copperbelt nchini Zambia eneo ambalo lina historia ndefu ya kisiasa na kiuchumi kutokana na uchimbaji madini, hasa shaba.
Edgar Chagwa Lungu alilelewa katika familia ya kawaida iliyoamini katika maadili ya dini ya Kikristo kutoka kwenye Kabila la Nsenga na kukulia katika mazingira ya miji ya viwandani, hali iliyomfundisha kutazama maisha ya wananchi wa kawaida na kumweka karibu na masuala ya kijamii.
Edgar Chagwa Lungu alipata elimu Shule ya Sekondari ya Mukuba huko Kitwe ,na kufanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu huku akihitimu shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Zambia (UNZA) mwaka 1981.
Katika Mafunzo ya Kitaaluma: Baada ya kumaliza chuo, alifanya mafunzo ya sheria (Legal Practicing Certificate) katika Chuo cha Sheria cha Zambia (ZIALE) na kuwa wakili.
Ingawa baada ya kuhitimu, Lungu alifanya kazi katika sekta ya umma kwa muda mfupi, kabla ya kujiunga na kampuni binafsi ya sheria, Andre Masiye and Company, ambako alifanya kazi kama wakili. Pia alijihusisha na shughuli za kidini na kijamii kama mshiriki wa Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA), akiwa mtu wa imani thabiti.
Katika miaka ya 80 na 90, alijaribu kuingia kwenye biashara lakini hakufanikiwa sana, na kwa muda fulani alielekea kuwa nje ya maisha ya umaarufu.
Edgar Lungu alianza harakati zake za kiasa kwa mara ya kwanza kama mwanachama wa chama cha United Party for National Development (UPND), lakini baadaye alijiunga na Patriotic Front (PF), chama kilichoasisiwa na Michael Sata mwaka 2001.
Katika hatua hiyo aligombea ubunge kwa tiketi ya kutoka chama cha PF na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Chawama mwaka 2011.
Baada ya ushindi wa Michael Sata kama Rais mwaka 2011 Lungu aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Usafirishaji, Utalii na Habari ,baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kisha Waziri wa Ulinzi, mnamo Mwaka 2013, pia alihudumu katika Wizaira ya Sheria kama kama waziri na hatimaye kuwa Kaimu Rais kwa muda mfupi wakati Rais Sata alipokuwa anaumwa.
Baada ya kifo cha Rais Michael Sata mnamo Oktoba 2014, Chama cha PF kilimchagua Lungu kuwa mgombea urais kwenye uchaguzi mdogo wa Januari 2015 na kufanikiwa kumshinda Hakainde Hichilema wa UPND kwa ushindi mwembamba.
Mnamo Mwaka 2016, Lungu alichaguliwa tena kwa kipindi kamili cha miaka mitano baada ya kumshinda tena Hakainde Hichilema ambapo kwa muda huo alikuwa Rais kamili aliyechaguliwa kwa uchaguzi wa kawaida.
Mafanikio ya Lungu katika sekta ya miundombinu katika kipindi cha uongozi wake , alisimamia ujenzi wa barabara nyingi, viwanja vya ndege (mfano, uboreshaji wa Kenneth Kaunda International Airport) na vituo vya afya.
Mradi wa ujenzi wa daraja la Kazungula (kuunganisha Zambia na Botswana) ulikamilishwa wakati wake.
Vilevile katika sekta ya nishati lungu alianzisha miradi ya kuongeza uzalishaji wa umeme, hasa kupitia mabwawa kama lile la Itezhi-Tezhi, aliboresha ushirikiano wa kikanda, hasa ndani ya SADC na COMESA.
Kutokana na hatua hizo zipo baadhi ya changamoto ambazo zilikuwa zikimkabili Edga Lungu katika kipindi chote cha uongozi wake zikiwemo:
• Kudidimia kwa Uchumi:
• Zambia ilikabiliwa na deni kubwa la taifa, kushuka kwa thamani ya Kwacha, na mfumuko wa bei.
• Nchi ilikumbwa na mgogoro wa madeni, hali iliyosababisha kuomba msaada wa IMF.
• Madai ya Ukandamizaji wa Demokrasia:
• Serikali yake ilishutumiwa kwa kuwakandamiza wapinzani, vyombo vya habari, na wanaharakati.
• Mnamo 2017, mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema alikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini — jambo lililokosolewa na jumuiya ya kimataifa.
• Utata wa Kikatiba:
• Lungu alihusishwa na juhudi za kutaka kugombea muhula wa tatu, ingawa alidai muhula wa kwanza wa 2015 haukufikisha miaka mitano kamili.
Mnamo Agosti 2021, Edgar Lungu alishindwa katika uchaguzi mkuu na Hakainde Hichilema wa chama cha UPND, ambaye alishinda kwa zaidi ya kura milioni 2.6 dhidi ya kura milioni 1.8 za Lungu jambo ambalo lilopelekea Lungu kukubali matokeo ingawa alidai kulikuwa na vurugu katika maeneo ya wafuasi wake.
Baada ya kuondoka madarakani, Lungu aliishi maisha ya kimya kimya kwa kipindi fulani. Hata hivyo:
• Alitangaza kurejea katika siasa mwaka 2023 kwa madai ya “kuendeleza mapambano ya kidemokrasia.”
• Serikali ya Hakainde Hichilema ilimwekea masharti kadhaa kuhusu ulinzi wake wa urais mstaafu ikiwa ataendelea kufanya siasa.
Edgar Lungu alikuwa kiongozi aliyeinuka kimya kimya kutoka uwakili hadi urais kupitia uaminifu wake kwa Michael Sata na chama cha PF hata hivyo Urais wake ulikuwa wa mafanikio ya miundombinu lakini pia ulizingirwa na changamoto kubwa za kiuchumi na ukosoaji wa kisiasa.
Edgar Lungu amefariki dunia mnamo juni 5,2025 akiwa na umri wa miaka 68 wakati akiendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Pretoria nchini Afrika Kusini huku sababu za kifo chake bado hajafahamika huku taarifa za kifo chake zimethibitishwa na familia yake pamoja na Chama chake cha PF.
Lungu aliongoza Zambia kwa miaka 6 kuanzia 2015 hadi 2021 na kushindwa katika uchaguzi na Rais wa sasa Hakainde Hichilema kwa kura nyingi Kiongozi huyo atakumbukwa kwa mengi nchini Zambia kutokana na mbinu zake za kiutendaji.
Ili kupata taarifa zaidi endelea kutufuatilia kupitia website yetu ya www.jembenijembe.com kupitia Instagram ,Facebook, tikok,x zamani twitter pamoja na YouTube