Kwa upande wa Serikali umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba inatarajia kuwa na Mashahidi 15 na vielelezo tisa katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu ambapo hayo yameelezwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini na Jopo la Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Nassoro Katuga baada ya kumsomea Lissu maelezo ya awali ‘Ph’.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi June 02, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa kwa Mashahidi wa upande wa Serikali huku Mawakili wa Lissu wakisema wao hawatataja sasa hivi idadi ya Mashahidi wao watako kuwanao.
Awali Lissu akisomewa PH alikana kwamba April 3, 2025 hakuitisha mkutano Makao Makuu ya CHADEMA kwa watia nia pia sio kweli kwamba vilialikwa vyombo vya habari kwa ajili ya kuhabarisha umma katika mkutano huo kwa maelezo hayo Lissu alikubali taarifa zake ikiwemo majina, yeye ni Mkazi wa Tegeta na kwamba na Mwenyekiti wa CHADEMA, pia alikubali kwamba ameshtakiwa Mahakamani hapo kwa makosa matatu ya kuchapisha taarifa za uongo.
Mbali na hayo, Lissu amekana kuchapisha taarifa za uongo kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mtaa 2024 Wagombea wa CHADEMA walienguliwa kwa maelekezo ya Rais, na kusema sio kweli kwamba Majaji ikiwa ni CCM hawawezi kutenda haki na kwamba wanataka kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani huku ikidaiwa maneno hayo alichapisha katika mtandao wa Youtube.