Majambazi wawili waliokuwa na visu waliingia katika shule ya upili nchini Uswidi siku ya Jumatatu na kuiba kompyuta za wanafunzi, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti.
Watu hao waliojifunika nyuso zao waliingia katika darasa la shule ya Vasteras wakati somo lilikuwa likiendelea.
Wanaume hao walichukua kompyuta zote za darasani lakini walilazimika kutupa baadhi baada ya walimu kuwafukuza.
Hakuna mwanafunzi au wafanyikazi waliojeruhiwa lakini mpita njia aliyejaribu kuingilia kati alipata kichapo kutoka kwa waliokuwa kwenye tukio.
Polisi hawakutoa maelezo kamili ya wizi huo lakini walisema maafisa walikuwa wameitwa kwenye eneo la tukio baada ya "wahalifu wengi" kuwalazimisha watu kupeana vifaa vya kielektroniki.
Tobias Ahlen, msemaji wa polisi wa eneo hilo, alisema maafisa wanashika doria katika eneo hilo.
Mkuu wa shule Henrik Pettersson alisema baadhi ya wanafunzi hawakujisikia vizuri wakati wa mchana.
"Kuna wengi ambao wamehuzunishwa, wamefadhaika na wameshtuka kushuhudia tukio la kutisha na la kuhuzunisha," aliambia gazeti la Aftonbladet.
"Jambo la aina hii halifai kutokea shuleni, ni mbaya," Bw Pettersson aliongeza.
Walio darasani na walimu waliowakimbiza majambazi wanapokea msaada, shule ilisema.