Wakuu wa Idara wa hospitali ya Rufaa ya
Kumbukumbu ya Mwl.JK Nyerere wametakiwa kuweka mkakati wa kuboresha
huduma za afya kwenye hospitali hiyo.
Hayo yamesemwa jana na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi wakati akiongea na
watumishi wa hospitali hiyo kwenye kikao cha pamoja ikiwa ni siku moja
baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuitembelea hospitali hiyo.
Prof.
Makubi amesema kuwa ni wakati sasa wa wakuu hao wa idara kukaa na
kujitathimini ili kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuboresha huduma za
hospitali hiyo kwani watu wanafuata huduma bora"lazima muanze
vizuri,mfanye kazi ili msije kuiangusha nyota mliyoletewa na
Rais,fanyani kazi kwa bidii kwani mpo kwenye fani sahihi".
Ameongeza
kuwa wakuu hao wa idara wanatakiwa wabebe majukumu yao, watumishi
wajitambue,wabadilike kifikra ili hospitali iweze kwenda mbele kwenye
utoaji wa huduma.
Hata hivyo Prof.Makubi hakusita kuwakumbusha
watumishi wa chini kufanya kazi kwa kujituma,kubadilika na kuwa walinzi
wa mali zilizopo kwenye hospitali hiyo na siyo kusubiri wakaguzi kutoka
nje .
"Huduma nzuri inaanzia getini,kujiandikisha na kila
eneo,kuweni na lugha nzuri,jipimeni kwa kutumia muda mfupi kwa
wagonjwa,mgonjwa afanyiwe vipimo vinavyohitajika,shikamaneni ili
tuimalize hospitali hii"Alisisitiza Prof. Makubi
Vile vile Katibu
Mkuu huyo hakusita kuwasisitiza watumishi hao kusimamia mapato ya
hospitali hiyo ili kuboresha huduma za hospitali hiyo na hata kwa wao
wenyewe watapata motisha na kuongeza morali ya kufanya kazi.