Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa kuwezesha
ujenzi wa madarasa 15,000 ili wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato
cha kwanza waweze kusoma bila msongamano.
Akiongea jana wakati
wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha
na kutibu maji Waziri Bashungwa amesema kwa wanafunzi waliokuwa
wakitembea umbali mrefu serikali imeweza kujenga shule shikizi 3000 ili
watoto hao waweze kupata elimu karibu na maeneo yao.
Amefafanua
kuwa kiasi cha shilingi bilioni 240 zimetumika katika ujenzi wa
madarasa 12,000, shilingi bilioni 60 zimetumika katika ujenzi wa shule
shikizi 3000 na shilingi bilioni 80 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa
mabweni ya watoto wenye mahitaji maalum nchini.
Bashungwa amesema
Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa
shule maalum za Sayansi kwa wasichana kwenye mikoa 10 ambapo mikoa 16
iliyobaki fedha zitatengwa kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 lengo likiwa
ni kuboresha sekta ya Elimu nchini.
Kuhusu elimu bila Malipo
Waziri Bashungwa amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kiasi cha
shilingi bilioni 312 zilitengwa kwa ajili ya elimu bila malipo ambapo
mpaka sasa ikiwa ni nusu mwaka kiasi cha shilingi 140.43 kimepelekwa
kwenye Mikoa yote nchini
Aidha, Waziri Bashungwa amesema katika
kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan kuhusu usimamizi na utekelezaji wa miradi ya
maendeleo,tayari amewasiliana na Ofisi ya Makaguzi Mkuu wa Serikali
(CAG) ili kutatua changamoto hiyo.