Wasira: "Sitaki Tena Urais , Mama Samia Suluhu Hassan Anatosha 2025"

Mwanasiasa   mkongwe nchini, Stephen Wasira, amesema Rais Samia aachwe amalizie vipindi viwili vya urais kama ilivyo utamaduni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliyasema hayo jana mkoani Mara alipopewa nafasi ya kuzungumza baada ya Rais Samia kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa chujio la maji wilayani Bunda.

“Wale waliosema wanataka urais 2025, mimi nawashauri wasubiri kwa sababu kwa utamaduni wa CCM kama kuna rais aliyepo ofisini huwa hatumpingi, tunampa nafasi amalizie awamu hiyo ambayo ni miaka 10,” alisema Wasira.

Alitoa mfano wake binafsi kwamba aliwania urais, lakini hakuupata na sasa kwa kuwa ameshapitwa na umri, amekaa pembeni na hana nia tena ya kuwania.

Wasira aliwataka wenye dhamira hiyo ya urais wasubiri hadi vipindi viwili vya Rais Samia vipite, na iwapo watakuwa wamepitwa na umri waige mfano wake, ambaye amejiunga na wazee wa Mara maana si wote lazima kuwa rais bali ni fursa ya mtu mmoja.

Akiongelea mradi wa maji alimpongeza Rais kwa kuwapatia fedha za mradi huo ulioasisiwa mwaka 1974 na hatua ya jana ndio inakamilisha ujenzi wa mradi huo.

Pia alimshukuru Rais kwa kuwapatia fedha za miradi mingine ya maendeleo ikiwamo kujengea shule, hospitali na maji katika mkoa huo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii