Namna Maboresho ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta yatakavyochochea Ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano Tanzania
KATIKA kuboresha
mazingira ya utoaji huduma za mawasiliano nchini Wizara ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wiki hii imetangaza maboresho ya
Kanuni za Miundombinu ya Utangazaji Dijiti na Kanuni za Leseni
zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Maboresho ya
Kanuni hizi pamoja na mambo mengine yanalenga kuboresha mazingira ya
uwekezaji na utoaji huduma nchini, na pia kupanua wigo wa upatikanaji wa
huduma za mawasiliano ya kielektroniki nchini.
Makala
haya yananuia kuainisha maboresho ya msingi yaliyofanywa kwenye Kanuni
mbili ambazo ni Kanuni za Leseni, 2018 na Kanuni za Miundombinu ya
Utangazaji Dijiti, 2018. Lengo la mabadiliko haya ni kuendana na
mabadiliko ya kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA).
Sehemu ya Kwanza: Maboresho katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Leseni), 2022
Katika maboresho haya mambo yaliyofanyiwa uboreshwaji ni kama ifuatavyo: -
Mosi;
Kufuta ada ya masafa kwa wenye miundombinu ya utangazaji wa televisheni
dijiti (MUX) ili kuleta nafuu kwa wawekezaji kwenye eneo hili na
kuwawezesha kupanua wigo wa huduma za Mawasiliano pamoja na kuhakikisha
upatikanaji wa huduma bora za Mawasiliano;
Pili;
kuainisha aina mpya ya leseni maalum kwa watoa huduma wanaotengeneza
bando za maudhui, kurahisisha utoaji wa leseni na pia kuhimiza
watengenezaji wa maudhui wa ndani kuandaa maudhui yanayohamasisha ukuaji
wa utamaduni wa Kitanzania na jamii inayoizunguka. Vilevile, kuongeza
ajira kwa vijana wanaovutiwa na uandaaji wa maudhui kwa kuzingatia kuwa
hitaji la soko katika miaka ya hivi karibuni limeongezeka kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la idadi ya watu.
Tatu;
kubadili leseni ya vituo vya utangazaji vya kijamii kuwa leseni ndogo.
Lengo la maboresho haya haya ni kuchochea uanzishwaji wa vituo vya
utangazaji vya kijamii kwenye maeneo ya nchi yasiyofikiwa au yanayopata
huduma hafifu za utangazaji hasa wa redio. Hatua hii pia itawezesha
wananchi kunufaika kwa kupata huduma za maudhui ya utangazaji
yanayoakisi maisha na tamaduni zao katika maeneo husika. Aidha
upatikanaji wa leseni hizi utachukua muda mchache zaidi kwa kuwa
mlolongo wa uchakataji wa leseni umefupishwa tofauti na leseni kubwa
ambazo zinahitaji mchakato wenye mlolongo zaidi hadi hatua ya mwisho ya
ukamilishwaji.
Nne;
kupunguza ada za leseni ili kuwezesha utoaji huduma nafuu na wenye
viwango utakaosaidia kukuza ajira na kuvutia watu wengi zaidi kuwekeza
katika sekta ya Mawasiliano nchini.
Tano;
kuainisha aina mpya ya leseni ya utangazaji kwa maudhui maalum ya elimu
ili kutoa nafasi kwa taasisi au mashirika yanayonuia kutoa huduma ya
elimu kutoa huduma hiyo kwa kuzingatia kwamba mazingira ya utoaji elimu
yamekuwa yakibadilika katika miaka ya karibuni kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo mkurupuko wa maradhi kama vile UVIKO-19 uliochagiza
kubadilika kwa modali ya uwasilishaji elimu maeneo mengi duniani,
Tanzania ikiwemo.
Sehemu ya Pili: Maboresho katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Redio na Televisheni), 2021
Maboresho
yafuatayo yamefanyika kwenye kanuni zinazoongoza huduma za utangazaji
wa Televisheni na Redio, kama ifuatavyo, Mosi; Kuruhusu chaneli za
televisheni za kulipia kuchukua matangazo ya kibiashara (yasizidi dakika
5 kwa saa). Kabla ya maboresho haya ya Kanuni, haikuruhusiwa chaneli za
televisheni za kulipia kuweka matangazo ya kibiashara.
Wizara
Pamoja na TCRA wanabainisha kwamba lengo la kuruhusu chaneli za
televisheni za kulipia ziweze kuchukua matangazo ya kibiashara ni kuweka
mazingira bora zaidi ya uwekezaji katika utengenezaji wa maudhui na pia
kuendana na uhalisia wa biashara ya chaneli za maudhui ya kulipia;
kuhimiza (promote) maudhui ya ndani na pia kuwezesha wasanii wa ndani
kutengeneza maudhui ya kulipia.
Nne;
Kuruhusu chaneli za televisheni za kutazamwa bila kulipia (Free to Air)
zioneshwe bila kulipia katika visimbuzi vyote nchini pasipo kujali ni
vya kulipia au la. Kabla ya maboresho haya ya Kanuni, chaneli za
kutazamwa bila kulipia (Free to Air) hazikuruhusiwa kuoneshwa katika
ving’amuzi vya kulipia nchini. Lengo la maboresho katika eneo hili ni
kuongeza wigo wa mapato kwa watoa huduma wa chaneli za kutazamwa bila
kulipia; kuongeza wigo wa ufikiwaji wa habari kwa wananchi kwani kwa
maboresho haya kila king’amuzi kitaweza kuonesha chaneli zote, za
kulipia na zisizo za kulipia.
Aidha
hatua hiyo ya kuruhusu visimbuzi vyote kubeba chaneli za bila kulipia
kunaongeza na kuwezesha uhuru wa watazamaji kuchagua chaneli watakazo
kirahisi; pia itawezesha kutatatua changamoto ya mtumiaji kulazimika
kumiliki kisimbuzi zaidi ya kimoja.
Mabadiliko
mengine kwenye Kanuni hizi ni yanayoruhusu chaneli za televisheni za
kulipia kurusha matukio mbashara (live events) yakiwemo matukio ya
kitaifa kama vile hotuba za Viongozi Waandamizi wa Taifa. Kabla ya
marekebisho haya chaneli za kulipia hazikuruhusiwa kurusha matukio
mbashara.
Sehemu ya Tatu: Maboresho katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Simu na Intaneti), 2021
Katika Kanuni hizi mambo kadhaa yamefanyiwa maboresho na marekebisho kama ifuatavyo Mosi;
Kwanza
ni kuboresha mfumo wa leseni kwa kuainisha leseni ya Vituo vya
Kuhifadhi Taarifa (Public Data Centre Licence). Maboresho haya yanalenga
kuongeza wigo wa uwekezaji katika huduma za mawasiliano hasa katika
masuala ya kuhifadhi taarifa kutokana na ongezeko la huduma mtandao kama
vile cloud computing services. Pili; kuainisha leseni kwa ajili ya
vituo vya maingiliano ya mtandao (Internet exchange Points). Maboresho
haya yatawezesha kuainisha vigezo vya kiufundi vya miundombinu ya vituo
vya maingiliano ya mtandao (Internet exchange Points).
Eneo
la tatu ni, kupunguza ada za masafa ya mawasiliano ya redio ili
kuhimiza upelekaji wa mtandao (network expansion) katika maeneo mengi
zaidi nchini. Mabadiliko haya yanaendana na Dira ya Maendeleo ya 2025
inayolenga kuhakikisha ufikishwaji wa huduma za TEHAMA kwa wananchi
wote. Maboresho ya nne yanahusisha kupunguza ada ya vituo vya
mawasiliano ya redio kutoka dola 3,000 na kuwa dola 100 kwa kituo, ili
kuongeza kasi ya usambazaji wa intaneti yenye kasi nchini hasa maeneo
yasiyofikiwa kirahisi na miundombinu iliyopo.
Tano;
kuainisha ada kwa ajili ya mawasiliano ya simu kwa njia ya setilaiti
ili kuongeza udhibiti wa huduma za mawasiliano ya simu kwa njia ya
setilaiti. Sita; kuondoa ada ya usajili kwa madishi ya mawasiliano ya
redio ili kuongeza usambaaji wa huduma. Saba; kupunguza ada za madishi
ya mawasiliano ya redio(VSAT) kutoka dola 3,000 na kuwa dola 60 ili
kuhimiza matumizi ya VSAT na pia kuchochea uwekezaji kwenye eneo hili.
Nane;
kutofautisha kati ya leseni ya kutengeneza vifaa vya mawasiliano ya
kielektroniki kwa mafundi wakubwa na wadogo. Mabadiliko ya tisa yanahusu
kupunguza ada mbalimbali za leseni, ili kupunguza mzigo wa ada kwa
watoa huduma na kuhimiza uwekezaji zaidi na mwisho kuongeza aina mpya ya
leseni ndogo kwa ajili ya huduma mtandao, ili kutambua huduma mpya za
mtandao na kuweka mazingira wezeshi kiudhibiti.
Maboresho
ya Kanuni ni suala muhimu katika kuhakikisha utoaji wa huduma za
mawasiliano unaendana na mabadiliko ya teknolojia na uhalisia wa
mazingira yaliyopo, ambapo dhamira ya Serikali ni kuendelea kufanya
maboresho ya Kanuni kila itakapohitajika kwa kuzingatia kuwa; teknolojia
inabadilika kila mara kama mkondo wa maji unavyobadili njia zake kila
mtiririko unavyosonga.
Wizara
ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Pamoja na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanatarajia kuona wadau wa sekta ya
mawasiliano wakiendeleza ushirikiano madhubuti ili kuendelea kuijenga
Tanzania yenye huduma bora za mawasiliano ambazo ni chachu ya maendeleo
ya nchi yetu katika kujenga Uchumi wa Kidijitali.
Makala hii imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii