Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda kamati maalum ya kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mfanyabiashara wa madini, mama wa mfanyabiashara huyo amesema anautaka mwili wa mwanawe aliodai unaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi.
Wakati huohuo, baba mzazi wa mkaguzi msaidizi wa polisi anayedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu, Gaitan Mahembe alisema jana kuwa sasa ana imani ya kupatikana kwa ukweli badala ya kuangalia upande mmoja.
Rais Samia alitoa agizo juzi wilayani Magu mkoani Mwanza akiwa njiani kuelekea Musoma mkoani Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika jana.
Juzi hiyo hiyo, Waziri Mkuu, Majaliwa aliunda kamati hiyo yenye watu tisa itakayochunguza tuhuma za mauaji hayo yanayodaiwa kufanywa na askari polisi na mauaji yaliyofanyika wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kamati hiyo inajumuisha maofisa kutoka mamlaka tofauti za Serikali zikiwamo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.