Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi
na Serikali umeridhia na kupitisha ombi la Tanzania la kutaka Kiswahili
kuwa lugha ya kazi katika Umoja huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewasilisha ombi hilo la
lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kazi katika mikutano ya
Umoja wa Afrika.
Dkt. Mpango ameongeza kuwa Kiswahili ni
miongoni mwa lugha za kiafrika zenye wazungumzaji wengi barani Afrika
ambapo takribani watu milioni mia moja wanakitumia Kiswahili pamoja na
wazungumzaji kutoka nje ya Bara la Afrika.
Kutokana na umuhimu
wa lugha hiyo Makamu wa Rais amesema tayari inatumika katika jumuiya
mbalimbali ikiwemo jumuiya ya Afrika Mashariki ,Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kufundishwa kwa lugha hiyo katika
nchi nyingi za Afrika Mashuleni.
Amesema tayari Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni
limetangaza tarehe saba Julai ya kila mwaka kuwa siku ya maadhimisho ya
lugha Kiswahili Duniani.
Mkutano huo pia umeichagua Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU)
Pamoja
na mambo mengine mkutano huo wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja Afrika (AU) nchi wanchama zimelaani vitendo vya uvunjaji katiba
uliopelekea mapinduzi ya kijeshi katika mataifa mbalimbali pamoja na
vitendo vya ugaidi vinavyoendelea katika mataifa mbalimbali barani
Afrika. Umoja wa Afrika umeasa majadiliano kuendelea katika nchi hizo
ili kurejesha utawala wa kiraia na kidemokrasia.
Katika
kupambana na Uviko19, Umoja wa Afrika umetoa rai kwa nchi kushirikiana
katika kukabiliana na janga hilo ikiwemo kuhakikisha chanjo zinapatikana
pamoja na kuyaunga mkono mataifa yalioanza jitihada za kuzalisha chanjo
hiyo barani Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Senagal na Rwanda.