Kiongozi mkuu wa upinzan nchini Kenya, Raila Odinga amefichua kuwa aliamua kumwokoa Rais William Ruto wakati wa maandamano ya Gen Z ili kuzima mapinduzi ya kijeshi ambayo yalikuwa yamesukwa na yalikuwa yakikaribia kutekelezwa.
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya alifunguka na kusema alipigiwa simu na ‘rafiki’ ambaye alimwomba aingilie kati kwa sababu jeshi lilikuwa likielekea kuung’oa utawala wa Rais Ruto iwapo maandamano yangeendelea kushamiri.
Raila alisema kuwa baada ya Bunge la Kitaifa kuvamiwa mnamo Juni 25, 2024 na vijana kuanza maasi yao kwa kulenga Ikulu, ilikuwa dhahiri kwamba utawala wa Kenya Kwanza ulikuwa ukielekea kuporomoka.
Hali hiyo ililazimu Rais kuagiza majeshi yatoke kwenye makao yao ili yahakikishe utulivu na amani vinakuwepo nchini baada ya polisi kulemewa na vijana.
“Ruto anaweza kuondolewa tu kupitia uchaguzi mkuu lakini unajua wanajeshi wakitoka kwenye kambi yao huwa hawarejei,” alisema Raila wakati wa mahojiano maalum jijini Nairobi.
Kiongozi huyo alifananisha hali ambayo Kenya ilijipata na yaliyotokea Misri wakati kundi la Muslim Brotherhood (Ikhwanul Muslimin) lilipomwondoa mamlakani Rais Hosni Mubarak.
Kiongozi huyo wa upinzani alisimulia jinsi alivyotumia ushawishi wake wa kisiasa kuhakikisha Rais anatupilia mbali Mswada wa Fedha 2024 ambao ulikuwa unapingwa na vijana nchini.
Kuhusu ushirikiano wa sasa na serikali ya Ruto, Raila ameutaja kuwa bora zaidi na mkataba walioutia saini na Ruto unalenga mshikamano nchini Kenya.