Watu 30 wameuawa katika eneo la Ruweng, Kaskazini mwa Sudan Kusini, baada ya kushambuliwa na vijana waliokuwa wamejihami kwa silaha.
Mauaji haya yameripotiwa kutokea baada ya mzozo kati ya wafugaji na wakulima, kwa mujibu wa walioshuhudia.
Makabiliano hayo yalianza mapema wiki hii, wakati kundi la vijana wenye silaha, walipoiba kondoo, wakati walipokabiliwa na maafisa wa usalama.
Uongozi wa serikali katika eneo hilo, wamethibitisha mauaji hayo na kuongeza kuwa wengine 40 wamejeruhiwa, wengi wakiwa ni kundi la vijana hao waliokuwa wamejihami kwa silaha.
Haya yanajiri katika nchi hiyo ambayo katika siku za hivi karibuni, imeendelea kukabiliwa na mzozo wa kisiasa baada ya kukamatwa kwa makamu wa kwanza wa rais Riek Machar.
Sudan Kusini imeendelea kukumbwa na utovu wa usalama tangu uhuru wake mwaka 2011 ilipojitenga na Sudan, licha ya nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali ya mafuta.