Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck amelihimiza taifa hilo kupunguza utegemezi wake wa gesi asilia kutoka Urusi wakati kukiwa na wasiwasi kuhusiana na mzozo wa Ukraine.
Matamshi yake yaliyochapishwa jana Jumamosi yanatolewa wakati mradi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2 wa kusafirisha gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani kupitia Bahari ya Baltiki ukiwa umesimama na ukikabiliwa na kitisho cha vikwazo.
Habeck amesema mzozo wa Ukraine unaisukuma Ujerumani kuangazia fursa nyingine za kuingiza nishati hiyo pamoja na kuongeza usambazaji ikiwa ni pamoja na masuala ya miundombinu.
Ujerumani inategemea zaidi ya theluthi ya gesi kutoka Urusi ili kukidhi mahitaji yake, wakati ikiachana na matumizi ya makaa na nishati za nyuklia