Kifo cha kiongozi wa Hamas: Kiongozi mkuu wa Iran aahidi 'adhabu kali' kwa Israeli

Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameapa siku ya Jumatano, Julai 31, kutoa "adhabu kali" kwa Israel, inayotuhumiwa kumuua kiongozi wa Hamas wa Palestina Ismaïl Haniyeh mjini Tehran.

"Kwa kitendo hiki, utawala wa Kizayuni unaojihusisha na mauaji na ugaidi umejitengenezea uwanja wa adhabu kali, na tunaona kuwa ni wajibu wetu kulipiza kisasi cha damu ya Haniyeh iliyomwagwa katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesema katika taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la serikali la IRNA.

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amelaani haraka katika taarifa yake "mauaji ya kutisha" ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, wakati Moussa Abou Marzouk, afisa katika ofisi ya kisiasa ya Hamas, amesema katika taarifa yake kwamba "kitendo cha kutisha, hakitapita bila jibu." 

Recep Tayyip Erdogan, rais wa Uturuki, kwa upande wake ameshutumu "mauaji ya kidhalimu" ya "kaka" yake Ismaïl Haniyeh.

Ismaïl Haniyeh, ambaye alijiunga na Hamas mwaka 1987, alijipatia umaarufu mwaka 2006 kwa kuwa Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina baada ya ushindi wa kushtukiza wa kundi lake katika uchaguzi wa wabunge. Alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas mwaka 2017, akimrithi Khaled Mechaal, na aliishi uhamishoni kwa hiari nchini Qatar.




Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii