• Alhamisi , Mei 1 , 2025

Wazalishaji mbegu feki wadakwa Magu, DC Nassari atoa ujumbe kwa wakulima


VIJANA wawili wamekamatwa na vyombo za ulinzi na usalama wilayani Magu mkoani Mwanza kwa tuhuma za kuzalisha na kusambaza mbegu feki za mahindi zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 41 pamoja na dawa feki za mifugo hali inayotajwa kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuwainua wakulima na wafugaji.

Vijana hao ndugu, Mahe James Raymond (28) na Omary James Mahe (27) wamekamatwa juzi Jumatano tarehe 23 Oktoba, 2024 na jeshi la polisi wilayani Magu kwa kushirikana na maofisa ukaguzi wa wilaya ya Magu baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Watuhumiwa hao ambao wanashikiliwa katika kituo cha polisi wilaya ya Magu, walikuwa wakiendesha shughuli zao za uzalishaji wa mbegu feki katika moja ya nyumba iliyopo mtaa wa Isandula Juu, kata ya Kandawe – Magu Mjini.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari amesema baada ya kupekua nyumba hiyo wamebaini zaidi ya magunia 20 ya mahindi ambayo yalikuwa yanaandaliwa kuwekwa rangi kabla ya kupakiwa kwenye vifungashio.

“Mfano mamlaka ya hali ya hewa (TMA) imesema mvua za vuli msimu huu zitakuwa za wastani na chini ya wastani, hivyo tulikuwa tunamshauri mkulima kulima mahindi kwa kutumia mbegu ambazo ni za muda mfupi lakini unaweza kumwambia mkulima anunue DK 777 za muda mfupi kumbe mbegu yenyewe ni feki hili ni kosa kubwa linarudisha nyuma jitihada za serikali kumkwamua mkulima,” amesema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii