Korea Kaskazini yakiri kupeleka wanajeshi kusaidia Urusi vitani Ukraine

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miezi saba, Korea Kaskazini imekiri rasmi leo Jumatatu, Aprili 28, kupitia shirika la habari la serikali KCNA, kwamba ilituma wanajeshi kusaidia vikosi vya Urusi kwenye mstari wa mbele nchini Ukraine. Ukraine inakadiria kuwa karibu wanajeshi 14,000 wa Korea Kaskazini wametumwa Kursk tangu mwezi Novemba 2024.

Baada ya kimya cha miezi kadhaa, utawala wa Korea Kaskazini umekiri kuingilia kati mzozo huo pamoja na vikosi vya Urusi kupitia vyombo vyake vya habari vya serikali. Pyongyang inadai kuwa kutuma wanajeshi wake ni mfano wa urafiki wake wa kistratijia na Moscow na kuwaita wanajeshi wake mashujaa.

Operesheni hii ya kuwatuma wanajeshi kusaidi vikosi vya Urusi nchini Ukraine ni ya gharama kubwa katika suala la maisha kwa serikali, ambayo tayari imepata hasara karibu wanajeshi 4,000. Kwa wanajeshi hawa waliouawa vitani nchini Ukraine, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ameahidi kuwajengea mnara wa kumbukumbu katika mji mkuu, Pyongyang, ambapo familia zinaweza kutoa heshima zao. Vladimir Putin, kwa upande wake, amemshukuru kiongozi wa Korea Kaskazini siku ya Jumatatu kwa "kuwaenzi" wanajeshi wake.

Uthibitisho kutoka Urusi

Utambuzi huu wa ushiriki wa Korea Kaskazini katika mzozo huo unakuja siku mbili baada ya Urusi pia kuthibitisha kuwepo kwa askari kutoka "serikali ya Korea Kaskazini" huko Kursk. Katika hotuba yake siku ya Jumamosi, Mkuu wa majeshi ya Urusi Valery Gerasimov alisifu "ushujaa" wa wapiganaji wa Korea Kaskazini waliotumwa na kuchukua tena udhibiti wa mkoa huo, uthibitisho wa kwanza rasmi kutoka kwa Moscow wa "kushiriki," kwa maneno yake, kwa askari hawa katika mgogoro huo unaolikumba eneo hilo.

"Wanajeshi na maafisa wa jeshi la Korea Kaskazini, ambao walipigana pamoja na jeshi la Urusi, walionyesha weledi mkubwa, uthabiti, ujasiri na ushujaa katika kuzima uvamizi wa Ukraine," alisema, akikaribisha "msaada mkubwa" uliotolewa.

Pia ni njia kwa Korea Kaskazini kurasimisha uingiliaji kati wake na kudai fidia ya kifedha kutoka Moscow. Akialikwa na Vladimir Putin, Kim Jong-un anaweza kuzuru Urusi katika wiki zijazo.

Kwa miezi kadhaa, Ukraine, Korea Kusini na nchi za Magharibi zimekuwa zikilaani ushiriki wa wanajeshi elfu kadhaa wa Korea Kaskazini katika mapigano hayo, jambo ambalo Moscow na Pyongyang hazijawahi kulithibitisha wala kukanusha. Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini kwa upande wake imeshutumu hatua hiyo siku ya Jumatatu na kusema ni ukiukaji wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. "Kwa kukubali rasmi, (Korea Kaskazini) imekubali vitendo vyake vya uhalifu," msemaji wa wizara amesema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii