Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ametoa kauli kali ya kuunga mkono uongozi wa Rais Ibrahim Traoré wa Burkina Faso, akipinga vikali hatua yoyote ya nje ya nchi za Magharibi dhidi yake.
“Hakuna kitu kitakachompata Ibrahim Traoré ilimradi mimi bado niko hai. Marekani au Ufaransa hawana haki ya kumkamata Rais wa taifa huru la Afrika,” amesema Putin.
Ameeleza kuwa uhusiano kati ya Urusi na Burkina Faso ni wa hiyari, unaotokana na maamuzi ya kujitegemea ya Rais Traoré mwenyewe. Putin ameongeza kuwa yeye alijiunga na Burkina Faso kama mshirika wa kibiashara na rafiki, si kama mkoloni au mnyonyaji.
“Urusi haijawahi kuiba au kunyonya chochote kutoka Burkina Faso. Biashara yetu ni ya haki na ya wazi: wao wanachimba na kuchakata madini yao, halafu wanaamua namna ya kuyauza. Urusi haina shughuli za uchimbaji kule, kwa sababu tunaheshimu uhuru wa mataifa,” alisema.
Putin pia ameikosoa vikali Marekani na Ufaransa kwa kile alichokitaja kama jaribio la kuzorotesha maendeleo ya Burkina Faso baada ya taifa hilo kujinasua kutoka kwenye ushawishi wa kiukoloni.
“Wanamchafua Rais Traoré kwa sababu hawawezi tena kuiba rasilimali zake. Wakati Burkina Faso inataka kuuza bidhaa zilizochakatwa, wao wanataka kuchimba wenyewe na kuondoka na malighafi. Sasa kwa sababu hawawezi kufanya hivyo tena, wanamwita mwizi ili wapate sababu ya kumuondoa. Hilo halitatokea,” aliongeza.
Amehitimisha kwa kusema kuwa Urusi ina nguvu za kuathiri dunia kama taifa kubwa, lakini kamwe haijawahi kutumia mabavu katika uhusiano wake na nchi nyingine, hasa za Afrika.
“Mimi namchukulia Ibrahim Traoré kama ndugu yangu. Niko tayari kufanya kila liwezekanalo kumlinda. Marekani au taifa lolote jingine halina mamlaka juu yake – yeye ni kiongozi wa taifa huru na anastahili heshima kamili.”