Wimbi jipya la joto nchini Morocco laua watu 21 ndani ya saa 24

Watu 21 wamefariki katika muda wa saa 24 katika mji wa Beni Mellal, katikati mwa Morocco, kutokana na wimbi jipya la joto linaloikumba nchi hiyo, katika kipindi cha mwaka wake wa sita mfululizo wa ukame, Wizara ya Afya imesema hivi punde siku ya Alhamisi.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (DGM) ilitangaza wimbi kali la joto kuanzia siku ya Jumatatu hadi siku ya Jumatano katika maeneo kadhaa, na halijoto ikifikia hadi 48°C, haswa katika mji wa Beni Mellal. Katika mji huu ulioko zaidi ya kilomita 200 kusini mashariki mwa Casablanca, ambapo kipimajoto bado kilionyesha karibu digrii 43 siku ya Alhamisi, watu 21 walifariki siku ya Jumatano, kulingana na Wizara ya Afya.


Vifo vingi vinahusu watu wanaougua magonjwa sugu na wazee, joto la juu limechangia kuzorota kwa hali yao ya afya na kuwasababishia kvifo, "kurugenzi ya afya ya mkoa imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.


Wizara ya Afya imetangaza hatua za kukabiliana na athari za joto, hasa kuanzisha "saa za kudumu ndani ya vituo vya afya katika mikoa iliyoathiriwa na kuongezeka kwa joto", pamoja na uhamasishaji wa wataalamu wa afya na "utoaji wa dawa na vifaa vya hospitali".


Wizara haikuweza kubainisha mara moja ikiwa hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya walioaga dunia baada ya wimbi la joto kali nchini. Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, hali ya joto inatarajiwa kushuka katika siku zijazo. Huko mji wa Marrakech (kusini), ambapo hali ya joto ilifikia digrii 45 siku ya Alhamisi, itapungua digrii 10 siku ya Jumapili, kulingana na DGM.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii