Namibia yagawa nyama za wanyamapori kwa watu wanaokabiliwa na njaa

Zoezi la serikali ya Namibia la kukusanya zaidi ya wanyapori 700 kukabiliana na ukame mbaya zaidi katika miongo kadhaa linaendelea, huku takriban wanyama 160 wakiwa tayari wameuawa, wizara ya mazingira ilisema Jumanne.

Serikali ilitangaza zoezi hilo wiki iliyopita ili kupunguza matumizi ya malisho na usambazaji wa maji, na kutoa nyama kwa ajili ya mpango wa kusaidia maelfu ya watu wanaokabiliwa na njaa kutokana na ukame.

Mpango huo unaotekelezwa na wawindaji wa kitaalamu, unalenga viboko 30, nyati 60, swala 50, tembo 83, nyumbu 100, elands 100 na pundamilia 300.

Wanyama wengi wako katika hifadhi za kitaifa za nchi hiyo.

Takriban wanyama 157 kati ya 723 waliopangiwa kuchinjwa wameuawa hadi sasa, msemaji wa wizara ya mazingira Romeo Muyunda aliiambia AFP.

Alisema muda itakaochukua kukamilisha zoezi hilo unategemea mambo mbalimbali.

“Lengo letu ni kutekekeza operesheni hii kwa muda wa kutosha huku tukipunguza kiwewe kadri iwezekanavyo. Ni lazima tutenganishe wanyama hao ili wawindwe na wale wasiowindwa,” Muyunda alisema.

Kwa kuheshimu marufuku ya kimataifa ya uuzaji wa pembe za ndovu, meno ya tembo waliouawa yatahifadhiwa katika maghala ya serikali.

“Hadi sasa wanyama 157 wa aina tofauti wamewindwa, wakitoa kilo 56,875 za nyama,” taarifa ya wizara ya mazingira ilisema.

Namibia ilitangaza hali ya dharura mwezi Mei kutokana na ukame, ambao umekumba nchi kadhaa za kusini mwa Afrika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii