Taifa Stars yawasili salama Misri

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imewasili nchini Misri salama huku Kocha Msaidizi, Hemed Morocco, akisema kuwa Tanzania ina nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo wake wa awali dhidi ya Uganda.

Stars imetua nchini humo tayari kuikabili Uganda itakayokuwa mwenyeji wa mchezo huo wa Mzunguuko watatu wa Kundi F wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ utakaopigwa Ijumaa (Machi 24).

Timu hiyo iliondoka nchini jana Jumapili (Machi 19) ikiwa na baadhi ya wachezaji, wakati nyota wanaokipiga Young Africans wakitarajiwa kuondoka nchini leo Jumatatu (Machi 20) kuungana na wenzao.

Akizungumza baada ya kuwasili Misri, Morocco, Kocha Morocco amesema timu imefika salama na leo itaanza mazoezi kujiandaa kuwakabili wapinzani wao.

Amesema timu ipo katika hali nzuri na ina morari wa mchezo, anaamini itafanya vizuri kabla ya kucheza mechi ya marudiano itakayofanyika nchini Aprili 4, mwaka huu.

“Timu imefika salama na wachezaji wapo katika hali nzuri, wengine wanaocheza Yanga wataungana nasi leo huku nyota wa kimataifa nao wakitarajiwa kuwasili kambini wakati wowote,” amesema Morocco.

Wachezaji walioondoka jana Jumapili (Machi 19) ni Aishi Manula, Beno Kakolanya (Simba), Datius Peter (Kagera Sugar), Yahya Mbegu (hefu) na David Luhende (Kagera Sugar).

Wengine ni Abdallah Mfuko (Kagera Sugar), Sospeter Bajana (Azam), Mzamiru Yassin (Simba), Yusuph Kagoma (Singida BS), Abdul Suleiman (Azam FC), Edmund Joh (Geita Gold), Khalid Habibu (KMKM FC) na Anuary Jabiri (Kagera) Sugar).

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii