Ruto atangaza rasmi kiti cha Chebukati kuwa wazi

RAIS William Ruto ametangaza rasmi kuwa wazi nafasi za mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na makamisha watano.

Alitoa tangazo hilo kupitia taarifa iliyochapishwa katika toleo maalum la gazeti rasmi la serikali lililotolewa Jumanne, Februari 14, 2023.

“Kwa kutekeleza mamlaka yaliyoko katika sehemu 7A ya Sheria ya IEBC, 2011 ikisomwa pamoja na aya ya kwanza ya Mpangilio wa kwanza wa Sheria hiyo, miye William Samoei Ruto Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini ninatangaza wazi nafasi za; Mwenyekiti na Makamishna watano wa IEBC,” Rais akasema kwenye tangazo hilo.

Hatua hiyo sasa inatoa nafasi kwa uundwaji wa jopo la uteuzi ambalo litaongoza mchakato wa kijaza nafasi hizo. Jopo hilo pia litajaza nafasi zingine ambazo zitatokea katika IEBC miaka ijayo.

Mwenyekiti wa zamani Wafula Chebukati na makamishna Boya Molu na Abdi Guliye waliondoka rasmi afisini mnamo Januari 17 baada ya kukamilisha muhula wao wa kuhudumu.

Watatu hao waliteuliwa rasmi mnamo Januari 2017 pamoja na wengine wanne waliojiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Aliyekuwa naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera na makamishna Justus Nyang’aya na Francis Wanderi walijiuzulu Desemba 2022 baada ya Rais Ruto kuunda jopo la kuchunguza ombi la kutaka wafutwe kazi.

Ni kamishna Irene Masit ambaye angali afisini, japo amesimamishwa kazi, baada ya kuhiari kuchunguzwa na jopokazi hilo linaloongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii