Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametaja leo kuwa na huzuni na wasiwasi kufuatia taarifa za Askofu Roland Alvarez kuhukumiwa kifungo cha miaka 26 jela huko Nicaragua.
Askofu Alvarez ambaye ni mkosoaji mkubwa wa utawala wa Daniel Ortega alipewa hukumu hiyo siku ya Ijumaa baada ya kukataa kupanda ndege kuelekea Marekani pamoja na wafungwa wengine 222 ambao pia ni wapinzani wa Ortega.
Askofu huyo amevuliwa pia uraia wa Nicaragua na kupelekwa katika jela ya Modelo.
Alvarez alikamatwa mwezi Agosti pamoja na makasisi wengine na watu kadhaa. Ortega aliamuru kuachiliwa huru kwa watu wengi ambao ni viongozi wa kisiasa, mapadre, wanafunzi na wanaharakati ambao walikuwa ni wafungwa wa kisiasa. Baadhi yao walilazimika kupanda ndege hadi Washington siku ya Alhamisi.