Rais Erdogan wa Uturuki akiri serikali yake ilipata changamoto kushughulikia tetemeko baya la ardhi

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Jumatano alikiri kwamba kulikuwa na matatizo jinsi serikali yake ilivyoshughulikia tetemeko baya la ardhi kusini mwa Uturuki, huku waathirika wakiwa na hasira na kufadhaishwa kutokana na timu za waokoaji kutowasili kwa haraka kwenye eneo la tukio.

Erdogan ambaye atagombea uchaguzi wa mwezi Mei, amesema wakati wa ziara kwenye eneo kulikotokea janga hilo kwamba shughuli za uokoaji sasa zinafanyika kama kawaida na kuahidi kuwa hakuna mtu atakayeachwa bila makazi, huku idadi ya vifo vilivyoripotiwa kote Uturuki na nchi jirani ya Syria vikiongezeka na kufikia 12,000.

Katika eneo la kusini mwa Uturuki, watu walitafuta makazi ya muda na chakula katika hali ya hewa ya baridi kali, na kusubiri kwa uchungu kuona familia na marifiki zao ambao pengine bado wamezikwa chini ya lundo la vifusi.

Waokoaji wameendelea kuwapata baadhi ya watu wakiwa hai.

Lakini Waturuki wengi walilalamika juu ya ukosefu wa vifaa, utaalamu na msaada kuwaokoa wale waliokwama chini ya vifusi, wakati mwingine hata wakisikia vilio vyao, vya kuomba msaada.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii