Shirikisho la soka duniani FIFA limefahamisha leo kuwa baraza lake "kwa kauli moja limeamua" kusitisha kwa muda shughuli za Shirikisho la Soka la India, kutokana na uingiliaji katika masuala ya soka na watu walio nje ya shirikisho hilo. Hatua hii ina maana India haitaweza kuandaa michuano ya kandanda ya Kombe la Dunia la Wanawake walio chini ya umri wa miaka 17, ambayo ilipangwa kufanyika Oktoba 11 hadi 30 mwaka huu wa 2022. FIFA imesema hatua hiyo inaweza kufutwa ikiwa kutaunda kamati mpya ya wasimamizi wa shirikisho hilo. Mnamo mwezi Mei, Mahakama kuu ya India iliivunja kamati ya uongozi wa shirikisho la soka (AIFF) na kuteua kamati ya watu watatu ya kurekebisha sheria za shirikisho na kuandaa uchaguzi.