Rais wa zamani wa Uruguay aliyeiongoza nchi hiyo kati ya mwaka 2010-2015 akijulikana kama ‘Rais maskini zaidi duniani’ kutokana na kuishi maisha yake ya kawaida kabisa, José Mujica, “Pepe”, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89.
Rais wa sasa Yamandu Orsi alitangaza kifo cha mtangulizi wake kwenye jukwaa la X: “asante kwa kila kitu ulichotupa na kwa upendo wako mkubwa kwa watu wako.”
Chanzo cha kifo cha mwanasiasa huyo hakijajulikana lakini alikuwa akiugua saratani ya umio.
Kwa sababu ya alivyoishi kwa namna ya kawaida tu kama rais, ukosoaji wake wa ulaji na mageuzi ya kijamii aliyoyakuza – ambayo, pamoja na mambo mengine, yalimaanisha Uruguay kuwa nchi ya kwanza kuhalalisha matumizi ya bangi kama burudani – Mujica alikua mwanasiasa mashuhuri Amerika ya Kusini na kwingineko.
Umaarufu wake duniani si wa kawaida ukizingatia ni nchi yenye wakazi milioni 3.4 pekee.
Ukweli ni kwamba, ingawa wengi walimuona Mujica kama mtu nje ya tabaka la kisiasa, haikuwa hivyo.
Alisema mapenzi yake kwa siasa, pamoja na vitabu na kufanya kazi, alirithi kutoka kwa mama yake, ambaye alimlea katika makazi ya watu wa tabaka la kati huko Montevideo.
Akiwa kijana, Mujica alikuwa mwanachama wa Chama cha Kitaifa, mojawapo ya vyama vya jadi vya kisiasa nchini Uruguay, ambavyo baadaye vilikuja kuwa upinzani wa mrengo wa kati kwa serikali yake.
Mujica aliwahi kutekwa mara nne na katika mojawapo ya matukio hayo, mwaka wa 1970, alipigwa risasi sita na kukaribia kufa.