Serikali mpya ya Somalia iliyoapishwa imemteua aliyekuwa naibu kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Shabaab, Mukhtar Robow kuwa Waziri wa Masuala ya Kidini.
Robow ambaye pia aliwahi kuwa msemaji wa Al-Shabab, aliteuliwa kujiunga na Baraza la Mawaziri na Waziri Mkuu mpya wa Somalia, Hamza Abdi Barre.
Waziri huyo ni mwanzilishi mwenza wa Al-Shabaab na alikuwa namba mbili katika tabaka la utawala kwenye kundi hilo.
Hata hivyo, alijiondoa kwenye kundi hilo mwaka wa 2015, baada ya mzozo kuibuka na aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo, marehemu Ahmed Abdi Godane.
Robow alitaja tofauti za kiitikadi kama sababu ya kujiondoa kwake na kuunda kundi lake ambalo lilikuwa likipigana dhidi ya Al-Shabab
Mnamo Agosti 2018, waziri huyo mpya wa Masuala ya Kidini, alijisalimisha kwa mamlaka ya Somalia na aliwekwa chini ya ulinzi kwa muda mfupi.
Si mgeni katika siasa za taifa hilo na amekuwa chini ya kizuizi cha nyumbani baada ya maafisa wa rais wa zamani kumkamata kutoka Baidoa ambako alikuwa akijaribu kusimamia ugavana wa eneo hilo mnamo Desemba 2018.