Mashauri ya ndoa na talaka 1,358 yamefunguliwa katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke (IJC) jijini Dar es Salaam katika kipindi cha kuanzia Novemba mwaka jana hadi Julai mwaka huu.
Idadi hiyo ni sawa na mashauri 220 yanayofunguliwa kila mwezi kituoni hapo, hali inayoonyesha kuyumba kwa taasisi nyeti ya ndoa, hasa mkoani Dar es Salaam.
Mashauri hayo ni miongoni mwa mashauri 4,267 yaliyofunguliwa katika kipindi hicho, kati ya hayo 2,911 yakihusu mirathi.
Hata hivyo, kituo hicho kimefanikiwa kunusuru ndoa 29 kati ya 80, ambazo wanandoa walifikishana hapo kwa ajili ya kuzivunja.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Naibu Msajili wa IJC, Mary Moyo, alisema mashauri yanayoongoza kufunguliwa katika kituo hicho ni ya mirathi ambayo ni 2,911, sawa na asilimia 62 ya mashauri yote, ikifuatiwa na mashauri 1,358 ya ndoa na talaka sawa na asilimia 38.
Kwa upande wa mashauri ya ndoa yaliyofunguliwa katika kipindi hicho, Moyo alisema mashauri yanayoongoza ni ya talaka, wanandoa kuomba kutengana, mgawanyo wa mali baada ya ndoa kuvunjika, matunzo ya watoto na sehemu wanakotakiwa kuishi watoto baada ya wazazi wao kutengana.
Alisema kati ya mashauri 1,358 ya ndoa, mashauri 1,127 ndiyo yaliyosikilizwa na kutolewa maamuzi, huku mashauri 231 yakiwa bado hayajatolewa uamuzi.
“Takwimu hizi ni tangu kituo hiki kilipoanza kutoa huduma Novemba, 2021 hadi Julai 19, 2022 na wanaokuja kupata huduma katika kituo hiki wengi ni wanawake ambao wamekuwa wakifungua kesi za ndoa, talaka, malezi ya watoto na upande wa wajane wamekuwa wakifungua kesi za mirathi,” alisema Moyo.
Kuhusu mirathi, Moyo alisema tayari wasimamizi wa mirathi 2,376, sawa na asilimia 82 wameshateuliwa na mahakama hiyo kukusanya mali na madeni katika kipindi hicho.
Alieleza sababu kubwa ya kituo hicho kupokea kesi nyingi kwa kipindi kifupi ni kutokana na kituo hicho kuhudumia mkoa mzima wa Dar es Salaam.
Tofauti na mahakama nyingine, kituo hicho kina ngazi tano za mahakama kwa pamoja, yaani Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, jambo ambalo limerahisisha watu kupata huduma kwa urahisi.
Wasemavyo wachambuzi
Kutokana na idadi hiyo ya kesi, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema, familia ni chanzo cha kuheshimika, kulindwa kwa haki za binadamu
‘‘Usipokuwa na familia imara, kuna uwezekano wa kukiukwa kwa haki za binadamu, hasa kwa watoto na wanawake. Tukiwa hatuna familia imara wanaoathirika ni wanawake na watoto na ndoa zinapovunjika watoto wanakuwa wamekwisha kuzaliwa lakini wanakwenda kukutana na kadhia hii. Taasisi ya familia inapoyumba, ni tatizo kwa jamii,” alisema.
Ole Ngurumwa aliongeza kusema: “Hili ni jambo muhimu na taifa lolote linaanza kuundwa na familia imara na haya ni madhara kwa taifa ikiwa tuna taasisi ya ndoa isiyokuwa imara.”
Alisema, wakati kesi hizo zikifunguliwa na hata zisizofunguliwa, jamii inapaswa kujiuliza chanzo ni nini na kwa nini tumefikia hapa.
‘‘Watu wanakwenda kwenye ndoa pasina mikakati ya kuwaandaa. Wengine wanaingia katika taasisi ya familia kwa kufuata mkumbo na kuwafanya kuingia kwa mihemko ya miili na mali tofauti na zamani. Lakini yawezekana hawa wanaopelekana huko ndio zao la wazazi wao kutengana nao wanapokuja kuwa wakubwa linawarudia au kufanya kile kile,” alisema.
Ukatili kwa wanandoa
Kwa upande mwingine, Dawati ya Jinsia la Jeshi la Polisi katika kituo hicho, lilisema kesi 122 zimefunguliwa, kati ya hizo, kesi 20 zimefunguliwa na wanaume ambao wamedai kufanyiwa ukatili na wake zao.
Akielezea jinsi wanaume wanavyoenda kupatiwa huduma katika kituo hicho, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Tatu Itale kutoka dawati hilo, alisema wamepokea kesi 122 na kati ya hizo, 20 ni za wanaume waliofanyiwa ukatili na wake zao.
Akifafanua kesi hizo 20 za wanaume alisema kesi nne kati ya hizo ni za kuomba talaka, tano za kukataa ndoa zao zisivunjike na tatu ni za kunyanyaswa na wake zao pindi wanapostaafu.
“Vipigo ndani ya ndoa vinasababisha wanandoa kwenda kuomba talaka, huku wengine wakiingia kwenye ndoa kama majaribio na matokeo yake wanaachana,” alisema Itele.
Naye, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Happiness Nyange alisema jumla ya mashauri 80 ya kuvunja ndoa yalifunguliwa katika ofisi hiyo, huku wakinusuru ndoa 29 kati ya hizo ambazo zilikuwa katika hatua ya kuvunjika.
Nyange alisema mbali na idadi hiyo, pia wamepokea kesi za watoto 17 ambao wameenda moja kwa moja katika idara hiyo kuwashtaki wazazi wao kwa kushindwa kuwalea na kuwatunza.
“Kati ya mashauri haya 80, mashauri 29 tumefanikiwa kunusuru ndoa zao na tunaendelea kuzifuatilia kwa karibu, huku mashauri yaliyobaki ambayo ni 51 tumeyarudisha kwenye mabaraza ya usuluhishi ya migogoro ya ndoa ngazi ya kata”alisema Nyange.
Nyange alibainisha baadhi ya sababu zinazochangia wanandoa kuachana ni kushuka kwa kipato miongoni mwa wanandoa na hivyo kusababisha kufanya ukatili kwenye familia.
Sababu nyingine, alisema wapo baadhi ya wanaume ambao kipato chao kikiongezeka, wanaanzisha uhusiano nje ya ndoa na hivyo kutelekeza familia.