Waziri mkuu aliyeondolewa madarakani nchini Pakistan,
Imran Khan, ameitaka serikali kutangaza uchaguzi mpya ndani ya siku sita
kutoka sasa ama aitishe maandamano makubwa ya umma yasiyo kikomo katika
mji mkuu Islamabad.
Akizungumza kwenye mkutano uliowakusanya maelfu ya wafuasi wake mapema
siku ya Alkhamis (Mei 26), waziri mkuu huyo aliyeondolewa
, amedai kuwa wafuasi wake watano wameuawa katika maeneo mbalimbali
ya nchi na serikali aliyoita ya vibaraka, akitishia kuendelea na
maandamano ya umma hadi matakwa yao ya kuitishwa uchaguzi mpya
yatakapotimizwa.
"Leo, watumwa wa Marekani na mafisadi wakubwa
kabisa wa Pakistan wanawaogopa wananchi. Wamefungia njia kwa makontena
kote Pakistan, wanazuwia watu wetu na wanawakamata watu wetu," alisema
Khan.
Ingawa serikali haijasema chochote kuhusu madai hayo,
lakini imetuma wanajeshi kulinda majengo muhimu, yakiwemo ya bunge na
ofisi ya Waziri Mkuu Shahbaz Sharif, anayeshutumiwa na Khan kuingia
madarakani kwa msaada wa kifedha na kimkakati wa Marekani.
Tayari
Khan ameshawasili mjini Islamabad na msafara wa maelfu ya wafuasi wake
wanaokisiwa kufika 25,000, tayari kwa kile alichosema ni maandamano
yasiyo kikomo hadi matakwa yao ya uchaguzi mpya yatakapotimizwa.
Serikali ya Waziri Mkuu Shehbaz Sharifilikuwa
imeapa kuwa ingeliwazuwia waandamanaji kuingia mji mkuu, ikiyaita
maandamano yao kuwa ni "jaribio la kuligawa taifa na kuleta machafuko."
Lakini
baada ya kikao cha dharura cha Mahakama ya Juu jioni ya jana, majaji
walitowa ruhusa ya maandamano hayo kufanyika kando ya mji wa Islamabad,
ingawa Khan alisema angelishinikiza kufika kwenye kitovu vya mji huo
mkuu.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Rana Sanaullah, aliwasihi
wananchi kutokujitokeza kwenye maandamano hayo, akisema kuwa umma wa
nchi hiyo umemkataa mcheza kriketi huyo wa kimataifa aliyegeuka kuwa
mwanasiasa.
"Watu wa Pakistan wamechaguwa kusalia majumbani mwao
badala ya kuwa sehemu ya maandamano haya ya vurugu. Watu wamekataa moja
kwa moja maandamano haya ya kiadui," aliwaambia waandishi wa habari
mapema Alkhamis.
Khan alianza vuguvugu lake la maandamano kuelekea Islamabad kutokea mji wa kaskazini magharibi wa Peshawar, iliko ngome yake.
Makabiliano
yaliripotiwa kwenye mji wa mashariki wa Lahore, wakati polisi wa
kutuliza ghasia walipotumia gesi ya machozi na kuwarejesha nyuma maelfu
ya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe wakati wakijaribu kuvuuka
daraja kwa ajili ya kupanda mabasi ya kuelekea Islamabad.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii