Halmashauri
kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, imemsimamisha Mwenyekiti wa chama hicho
Taifa, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti wake Bara, Angelina Mtaigwa,
kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ukiukwaji wa maadili.
Uamuzi huo
umetangazwa Jumamosi, tarehe 21 Mei 2022 na Mwenyekiti wa kikao cha
halmashauri hiyo kilichoketi jijini Dar es Salaam, Joseph Selasini.
Akisoma
maazimio ya halmashauri hiyo, Selasini amedai Mbatia amesimamishwa
katika wadhifa huo kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri na makatibu
wake.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Martha Chiomba,
alidai kulazimishwa kujiuzulu na Mbatia, tuhuma ambazo mwanasiasa huyo
alizikanusha.
“Tulielezwa jinsi ambavyo mwenyekiti alimtaka
katibu mkuu ajiuzulu na ikumbukwe hana zaidi ya mwaka ndani ya chama na
katika mjadala tumekubaliana alikuwa anabadilisha makatibu wakuu jinsi
anavyotaka. Sasa huyu ni katibu wa sita tangu alivyokuwa mwenyekiti,”
amedai Selasini.
Selasini ametaja sababu nyingine za Mbatia
kusimamishwa, akidai anatuhumiwa kwa kukisabisha chama hicho kisishiriki
mikutano mbalimbali iliyotitishwa kwa ajili ya kujadili masuala ya
demokrasia ya vyama vingi, ikiwemo ulioitishwa na Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Amedai,
awali chama hicho kilikataa kushiriki vikao hivyo hadi Serikali
itakapokuwa na nia njema dhidi ya viongozi wa vyama vya siasa vya
upinzani, ikiwemo kuachwa huru kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
aliyekuwa rumande katika Gereza la Ukonga, kwa tuhuma za ugaidi.
Selasini
amedai, baada ya Mbowe kuachwa huru Machi 2022, NCCR-Mageuzi haikuwa na
kikwazo cha kushiriki vikao hivyo lakini Mbatia aliitisha kikao cha
kamati cha dharura kubatilisha uamuzi huo.
Selasini amedai
maazimio ya halmashauri hiyo kumsimamisha Mbatia ni halali, kwani akidi
ya wajumbe wake ilikidhi matakwa ya kisheria ambapo waliohudhuria ni 52
kati ya wajumbe 82.
“Kabla ya mjadala haujaanza ulizuka mjadala
wa Mwenyekiti wa chama kutokuwepo katika mkutano huu na taarifa
ilitolewa kwamba anazo taarifa za mkutano akishiriki kuuitisha na baada
ya kusubiri kwa muda bila kujulikana na wajumbe wako tayari ukumbi
tukaona mkutano uendelee,” amesema Selasini.