Idara ya mahakama ya Guinea imeanza uchunguzi dhidi ya rais wa zamani wa nchi Alpha Conde na maafisa wengine 26 waliokuwa katika serikali yake. Hatua hiyo inafuatia malalamiko kutoka kwa kundi moja la kiraia ambalo wakati mmoja lilipinga Conde kuitawala nchi hiyo kwa muhula wa tatu. Conde aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo Septemba 5 mwaka uliopita na akatiwa nguvuni. Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS iliusimamisha uanachama wa Guinea na kuiwekea vikwazo nchi hiyo kufuatia mapinduzi hayo. Rais wa mpito Mamady Doumbouya aliyeongoza mapinduzi hayo hivi karibuni alitangaza kuwa nchi hiyo itarudi katika utawala wa kiraia baada ya kipindi cha mpito cha miezi 39. Conde aliingia madarakani mwaka 2010 wakati ambapo Guinea ilifanya uchaguzi wake huru wa kwanza tangu ilipopata uhuru mwaka 1958.