Matajiri na maskini wanavyoishi sawa mtaani

Matajiri na maskini sasa wanaishi katika mazingira yanayowiana, hivyo ndivyo inavyoweza kuelezwa kwa kile kinachoonekana katika jamii huku wafanyabiashara wakijaribu kuweka usawa wa maisha kwa watu wenye uwezo mkubwa na wenye vipato vya chini.

Usawa huu unaowekwa na wafanyabiashara umeweza kuondoa tofauti ya maisha wanayoishi watu wa matabaka hayo mawili, huku wananchi wenye kipato cha chini wakirahisishiwa maisha zaidi.

Hapo awali kulikuwa na tofauti kubwa ya maisha katika maeneo yanayoonekana wanaishi watu wenye vipato vikubwa kuanzia kwenye bidhaa wanazotumia hadi maisha ya kila siku, sasa hivi mambo yamebadilika, hata maeneo wanayoishi watu wenye vipato vya chini wanapata bidhaa zinazouzwa kwa watu wenye vipato vikubwa.

Vitu kama mkate, kuku, siagi na aina mbalimbali za vyakula vikiwemo biriani, pilau, mazao ya baharini kama pweza na kamba ilikuwa nadra kuonekana uswahilini, lakini sasa vimesogezwa huko katika mtindo ambao hata mwenye kipato cha chini anaweza kumudu.

Mwandishi wa gazeti hili alifika eneo la Magomeni katika mtaa wa Idrisa, ambapo kuna maduka maarufu kwa uuzaji wa bidhaa mbalimbali kwa rejareja. Alishuhudia baadhi ya watu, hasa wanawake wakiwa wananunua mahitaji mbalimbali.

Muuzaji wa moja ya maduka hayo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema mahitaji ambayo hununuliwa sana maeneo hayo ni mkate, taulo za kuhifadhia watoto (pampas), viungo mbalimbali vya chakula, maziwa ya unga ya kupima na bidhaa nyinginezo.

Sakina Amiri, mteja aliyekuwa ametoka katika moja ya maduka hayo kununua alisema yeye ni mkazi wa Jangwani, lakini amefika hapo kufuata unafuu wa bidhaa.

“Kwa mfano hapa nimenunua siagi robo kwa Sh1,500 ambayo kabla ya kupanda kwa bidhaa ilikuwa Sh1,000, samli robo Sh1,000, mkate nusu Sh600 na maziwa ya kupima robo kwa Sh3,000,” alisema.

Majira ya saa 11:30 jioni Mwananchi lilifika katika eneo la Kigogo na kushuhudia pembezoni mwa barabara kukiwa na meza za wafanyabiashara wanaouza samaki, kuku na mboga za majani.

Mmoja wa wafanyabiashara wa kuku ambaye hakutaka kutajwa jina alieleza kuwa asilimia kubwa ya wateja wake hununua kuku ambao wamekatwa vipande.

“Biashara yangu kwa asilimia kubwa inaisha kwa kuuza kwa kugawa vipande kama nusu ambacho awali kilikuwa kinapatikana kwa Sh3,500 lakini baada ya vitu kuwa bei ninauza kwa Sh4,000, kuku mzima nauza mara chache sana, hasa kipindi cha karibia na sikukuu. Hapa kwa mimi binafsi mteja baada ya kuchagua kipande chake akipenda namfanyia na huduma ya kukaanga yeye akifika ni kuunga tu kwa gharama hiyohiyo,” alisema.

Maisha haya sasa yameshaanza kuzoeleka, jambo ambalo linawawezesha watu kula kile wanachokipenda, kwani hata wanapokuwa na hamu ya kula nyama ya kuku hawana ulazima wa kuwa na Sh7,000 au Sh15,000 ya kununua kuku wa kienyeji.

Japokuwa ni ngumu kukuta mtu akiuza kuku wa kienyeji kwa vipande, lakini kwa wale wa kisasa kila mtu anao uwezo wa kula hata akiwa na Sh1,500.

Hiyo ni kutokana na kuku hao kuuzwa kwa vipande na bei tofauti kulingana na ukubwa katika maeneo tofauti.

Eneo la Tabata Relini maarufu Tabata dampo ndiyo biashara kubwa inayochangamkiwa, hususan inapofika jioni na hufanyika hadi saa sita usiku.

Eneo hilo hujaa meza nyingi zikiwa zinauza kuku wa vipande kwa bei za Sh1,500 kwa paja moja, Sh2,000 kidari, mtu akitaka nusu kuku atauziwa kwa Sh3,500 na kuku mzima kwa Sh7,000.

Biashara hii inapochangamka watu wa hali tofauti za maisha hufika eneo hilo kujipatia kitoweo hicho ambapo kwa wale wanaotaka kutengeneza wenyewe nyumbani huuziwa ikiwa nyama mbichi huku wengine wakikaangiwa kabisa.

“Bei ni moja, iwe unachukua kipande kilichokaangwa au ambacho hakijakaangwa, kinachofanyika ni kumpa mteja tu nini anataka. Unajua hii imerahisisha watu wa vipato vyote kula kuku, isingekuwa na faida tusingefanya muda wote, japokuwa kuna wakati inaathiriwa na kupanda kwa bei ya kuku kutoka kwa wafugaji lakini bei ya huku mtaani inabaki vilevile,” alisema Abdul Issa.

Hilo limeonekana pia Tabata ambapo njia hiyo imekuwa ikitumika ili kurahisisha maisha ya watu kwa kupunguza gharama kubwa wanazoweza kupata vitu vizima na kuwapatia namna wanayoweza kuvipata kwa uchache wake.

Badala ya kuuza samaki mzima au kwa kilo kama huku mtaani wanakata vipande na kuuza kati ya Sh1,500 na Sh2,000.

Samaki hao huwa wamekaangwa kabisa, hivyo kuweka urahisi kwa wanunuzi kuchagua kula bila kupika tena au kupika vile wanavyotaka.

Kwenye suala la lishe maeneo tofauti hawatofautiani sana na hawapo nyuma, inawezekana sasa hivi maeneo hayo ndiyo yanaongoza kwa watu kula matunda ya aina mbalimbali kwa wakati mmoja kwa kuwa yanauzwa kwa vipande hivyo gharama yake huwa nafuu.

Katika baadhi ya maeneo matikiti maji huuzwa kwa kati ya Sh200, Sh500 na Sh1,000, huku nanasi na parachichi vikiuzwa kwa Sh200 kwa kipande.

Hali hii imekuwa ikiweka urahisi kwa wakazi wa maeneo haya kupata kile wanachokihitaji kwa gharama nafuu wao na familia zao.

“Kuna mwingine anakuja ukimuambia tikiti maji Sh2,000 hana hiyo hela, lakini akikuta vipande kama hivi vya Sh200 au 500 ni rahisi kwake kununua au mwingine anakuambia yuko peke yake hawezi nunua zima, hivyo hii inakuwa njia ya kumsaidia, lakini si hivyo tu, bajeti aliyonayo inakuwa haimruhusu kununua kitu kizima, hivyo anatamani hata kukipata kwa uchache wake.

Mbali na matunda, pia hata mikate kuna watu hawana uwezo wa kununua huu mzima wa Sh1,400 hivyo atakuja atataka umpe nusu kwa Sh700. Kuna wengine huwa wanakuja hadi na 350 wanataka robo,” alisema Andrew Joseph, muuzaji matunda Tabata St Marys.

Upande wa nepi za watoto pia ni tofauti na zamani ambapo wanawake walilazimika kuchana vitenge au kanga zao za zamani kuwavalisha watoto ili nguo zisichafuke wanapojisaidia.

Kwa sababu hiyo, wanawake wengi hivi sasa wamekuwa wakilazimika kutunza walau Sh500 kwa siku ili kupata nepi za watoto angalau moja ya kulalia mtoto wakati wa usiku.

“Ukimvisha hii hadi asubuhi, hamna kuhangaika tena kama zamani akiloanisha kitanda mtaamka wote ili mbadilishe mashuka, hata vitanda vyetu sasa vinakuwa havina harufu ya mikojo” alisema Ruth Bernard, mkazi wa Kisemvule.

Kwa mujibu wa Majaliwa Mashaka ambaye ni muuza duka, wamama wengi wamekuwa wakinunua nepi hizo kwa rejareja ambazo kiuhalali zilipaswa kuuzwa kwenye boksi kwa gharama ya kati ya Sh5,000 hadi Sh20,000 kulingana na kampuni.

Ubunifu umekwenda hadi kwenye bidhaa za jikoni, zimerahisishwa namna mtu anavyoweza kupata na kufurahia chakula anachokipika, viungo hivi pia vinapatikana kulingana na pesa ya mteja, kwani wauzaji wamekuwa tayari kumpatia mtu kitu anachohitaji.

Bidhaa zinazotumika jikoni mfano karoti na pilipili hoho zinauzwa kwa nusu bei. Mfano karoti nzima bei yake ni Sh200, kama mteja hana basi itakatwa mara mbili na kuuziwa kipande kimoja kwa Sh100, vivyo hivyo kwa hoho.

Mboga za majani nazo zinapatikana gharama nafuu, tena zikiwa tayari zimeshaandaliwa kwa kwenda kupikwa, hivyo mteja akifika anachukua na kwenda kupika.

Mfanyabiashara wa mboga katika soko la Mbagala, Rehama Ng’itu alisema: “Tunafanya hivi kurahisisha maisha, siku hizi watu wako busy na mambo mengi anaweza asipate hata muda wa kutwanga kisamvu na huko kwenye masupermarket bei juu, hivyo basi kwa kuwa tunataka kuuza tumeona isiwe tabu, wacha na sisi tutwange tuweke kwenye mifuko waje wachukue kazi yao iwe kupika tu”.

Kinachoendelea Dar es Salaam hakitofautiani na hali ilivyo jijini Mwanza, ambapo wafanyabiashara katika mitaa mbalimbali wamebuni mbinu ya kuuza kwa kibaba ili kuwafikia hata wasio na uwezo wa kununua kwa kilo moja, nusu na hata robo.

Miongoni mwa mazao yanayouzwa bei ghali ni karanga zinazouzwa Sh3,500 kwa kilo moja, njegere Sh5,000 kwa kilo moja, sukari inayouzwa kati ya Sh2,800 hadi Sh3,000, huku nyama ikiuzwa kati ya Sh7,500 hadi Sh8,000 kutegemeana na eneo pamoja na kitoweo cha samaki kinachouzwa Sh7,000 kwa samaki wa wastani.

Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wameanza kuuza karanga mbichi kuanzia Sh500 kwa kikombe kidogo kimoja na za kusagwa Sh500 kwa kipimo cha vijiko vinne vya kulia chakula, njegere nazo zikipimwa kikombe kimoja kidogo cha chai kwa Sh1,000, huku samaki wabichi wakiuzwa kwa vipande na nyama kuanzia Sh1,000 kulingana na hitaji la mteja.

Mfanyabiashara wa duka la nafaka Kata ya Butimba jijini Mwanza, Hemed Ali alisema: “Tunatofautiana vipato, kuna wengine hawana uwezo wa kununua kilo moja ya sukari kwa Sh2,800 lakini wanaweza kununua kipimo cha Sh300 na wateja wa aina hii ninao wengi kulingana na hali ya maisha ilivyo,” alisema

Naye Hawa Swedi, mkazi wa jijini humo alisema bidhaa kuuzwa kulingana na fedha ya mteja inapunguza makali ya mfumuko wa bei, hasa kwenye mahitaji muhimu kama mafuta ya kula, sukari na karanga katika mwezi wa Ramadhani.

Hali kama hiyo ipo pia mkoani Kilimanjaro, ambapo katika kukabiliana na ugumu wa maisha, wafanyabiashara wa maduka na magenge wamebuni namna bora ya kumhudumia kila mwananchi ili kumwezesha kumudu gharama kulingana na fedha aliyonayo.

Joyce Saria, mkazi wa Majengo alisema utaratibu huo angalau umewapunguzia ugumu wa maisha kutokana na kwamba bidhaa nyingi zimepanda bei, hali ambayo inawafanya kila siku maisha yanakuwa ni magumu.

“Tunashukuru sasa hivi baadhi ya wafanyabiashara wa maduka wameelewa namna ya kuhudumia wateja wa kila aina, kwa mfano sasa hivi ukienda dukani kipande cha sabuni kimepanda bei kutoka Sh500 hadi Sh700, lakini sasa hivi hiki hiki kipande cha sabuni kimepunguzwa ukubwa na unauziwa kwa Sh500,” alisema Joyce.

Jijini Mbeya imeelezwa kuwa uwepo wa wajasiriamali wanaokaanga vitoweo vya nyama ya kuku na kuuza kwa mfumo wa vipande umeondoa ushindani na kutofautisha familia tajiri na maskini jijini humo wanaoishi nyumba za kupanga.

Ulaji wa nyama ya kuku awali wananchi wa kipato cha chini walishindwa kumudu na kutegemea siku za sikukuu za mwisho wa mwaka, lakini sasa imekuwa tofauti ambapo wajasiriamali wanawake na wanaume wametumia fursa ya kuuza kwa mfumo wa vipande kwa bei ya Sh 500 mpaka 2,000 kulingana na ukubwa.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakazi wa Mtaa wa Simike walisema kuwa awali walikuwa wakishindwa kuwa wavumilivu na kulazimika kuingia kwenye mikopo au kuuza mazao ili kuweza kununua walau kwa siku za sikukuu za mwisho wa mwaka kula kitoweo hicho na familia.

“Kwa sasa tunapozungumzia nyama ya kuku ni kama tunapoenda kununua mboga za majani sokoni, kwani wafanyabiashara wametukomboa na kutusaidia hata kwa familia zetu kujenga heshima, kwani ukinunua vipande vya 2,000 vinakidhi mahitaji ya familia na wengi ndoa zetu zimeboreka,” alisema Rehema Mwanjonde.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii